Kampuni ya TikTok ya China kumshtaki Rais Trump wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63028-kampuni_ya_tiktok_ya_china_kumshtaki_rais_trump_wa_marekani
Kampuni ya TikTok ya China imefungua kesi ya kupinga amri ya Rais Donal Trump wa Marekani inayozuia shughuli zozote za kampuni mama ya kampuni ,ByteDance, kuendesha shughuli zake nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2020 22:18 UTC
  • Kampuni ya TikTok ya China kumshtaki Rais Trump wa Marekani

Kampuni ya TikTok ya China imefungua kesi ya kupinga amri ya Rais Donal Trump wa Marekani inayozuia shughuli zozote za kampuni mama ya kampuni ,ByteDance, kuendesha shughuli zake nchini Marekani.

Nyaraka za mashtaka zinaonyesha kuwa walioshtakiwa ni Rais Trump, Waziri wake wa biashara Wilbur Ross na Wizara ya biashara.

Kampuni ya TikTok inaishutumu serikali ya Marekani kwa kukiuka haki za kampuni hiyo bila ushahidi wowote, na kutoa amri ya serikali bila kufuata utaratibu wa kipengele cha tano cha katiba.

Kampuni ya TikTok imesema amri hiyo ni matumizi mabaya ya sheria ya nguvu ya uchumi ya kimataifa (IEEPA) kuzuia shughuli ambayo "sio tishio lisilo la kawaida".

TikTok imesema amri hiyo ni "amri ya kisiasa na sio tishio lisilo la kawaida kwa Marekani" ambalo linatakiwa kuwa msingi wa rais wa Marekani kutoa amri kama hiyo.

Vita baridi baina ya China na Marekani vilishadidi baada ya Tump kutangaza kwamba anapiga marufuku nchini humo aplikesheni ya video maarufu ya TikTok inayomilikiwa na China.

Maafisa wa usalama wa Marekani wanadai kwamba aplikesheni hiyo ya kampuni ya ByteDance ya China, inaweza kutumiwa kukusanya data binafsi za raia wa Marekani.

Hatahivyo, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limetangaza kuwa halina ushahidi wowote unaothibitisha kwamba serikali ya China inapata taarifa binafsi za raia wa Marekani kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok.

Gazeti la New York Times hivi karibuni limeripoti kuwa, wachambuzi wa shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, wameandika katika ripoti iliyotumwa White House kwamba "hakuna ushahidi wowote" unaothibitisha kwamba serikali ya China imefanya jitihada za kudukua na kupata taarifa binafsi za watumia wa mtandao wa TikTok.