Iran yataka Saudi iwajibishwe kwa shughuli zake za siri za nyuklia
Mwakilishi wa Iran katika Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kubebeshwa dhima Saudi Arabia kutokana na kuendesha shughuli zake za nyuklia kwa siri na kificho.
Heidar Ali Balouji amesema hayo katika radiamali yake kwa madai na tuhuma zisizo za msingi za watawala wa Riyadh dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akijibu matamshi ya kijuba yaliyotolewa hivi karibuni na Abdullah al-Moallem, Mwakilishi wa Kudumu wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa, Balouji amesema inasikitisha kuona nchi kama Saudia inaibua madai ya uhasama dhidi ya Iran, katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikitoa mapendekezo na kubuni mipango ya amani kwa ajili ya uthabiti wa eneo hili la Asia Magharibi.
Ameongeza kuwa, badala ya Saudia kuafiki mipango ya amani inayobuniwa na Iran, imeng'ang'ania sera yake iliyofeli ya kujaribu kusuluhisha migogoro kwa njia za kijeshi huku ikiibua madai yasiyo na msingi dhidi ya Tehran.
Mwakilishi huyo wa Iran katika Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la UN ameeleza bayana kuwa, Iran daima imekuwa muwazi katika shughuli zake za nyuklia, na ni kutokana na ukweli huo ndio maana Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishatia ya Atomiki IAEA hivi karibuni akayataja makubaliano mapya baina Tehran na IAEA kama 'wasaa bora katika diplomasia'.
Ameitaka Riyadh iwache usiri katika shughuli zake za nyuklia, na iwaruhusu wataalamu wa IAEA wakague miradi yake hiyo. Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa ishirikiane kuhakikisha kuwa vituo vya nyuklia vya Saudia vinamtabuliwa na kujulikana wazi, na iilazimishe Riyadh iheshimu sheria na kanuni za wakala wa IAEA.