Iran yachukua uwenyekiti wa Kundi la 24
Gavana wa Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kundi la 24 (G24) katika kikao cha mawaziri wa fedha na magavana wa benki wa nchi wanachama kilichofanyika kwa njia ya intaneti.
Abdolnasser Hemmati, Gavana wa Benki Kuu ya Iran amehutubu baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kundi la 24 ambapo ameishukuru Ghana kwa uwenyekiti wake wa mwaka uliopita wa kundi hilo. Amesema kwa kuzingatia hali mbaya ya kiuchumi duniani iliyosababishwa na janga la corona, majukumu ya Kundi la 24 yanazidi kuwa muhimu siku baada ya siku.
Hemmati amesisitiza kuhusu ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kutatua matatizo hasa yanayohusu janga la corona na kuongeza kuwa, Kundi la 24 limekuwa likiunga mkono ushirikiano wa kimataifa katika utatuzi wa matatizo yaliyopita. Aidha amesema nchi zote duniani zinapaswa kuwezeshwa kupata chanjo na tiba isiyo ghali ya corona hata kama itabidi zipewe msaada wa dharura.
Gavana wa Benki Kuu ya Iran ametoa hakikisho kuwa, katika uwenyekiti wake atahakikisha kuwa Kundi la 24 linatunga sera za muda mrefu sambamba na kuzisaidia nchi wanachama kukubiliana na janga la corona.
Kundi la G24 liliundwa mwaka 1971 kama tawi la kundi la G77 la nchi zinazostawi na lengo lake ni kuratibu sera na ushirikiano wa nchi zinazostawi katika masuala ya kifedha na kuhakikisha maslahi ya nchi hizo yanawasilishwa katika mazungumzo ya kimataifa ya masuala ya fedha. Hivi sasa wanachama wa kundi hilo wamefika 28. Nchi wanachama ni kutoka maeneo ya Afrika, Amerika ya Latini, Karibia na Asia.