Uingereza yasema iko tayari kujitoa Umoja wa Ulaya bila kufikia makubaliano
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64092-uingereza_yasema_iko_tayari_kujitoa_umoja_wa_ulaya_bila_kufikia_makubaliano
Waziri wa Uingereza anayesimamia mchakato wa nchi hiyo kujitoa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama BREXIT ametangaza kuwa nchi yake iko tayari kujitoa katika umoja huo bila kufikiwa mwafaka kamili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2020 11:16 UTC
  • Uingereza yasema iko tayari kujitoa Umoja wa Ulaya bila kufikia makubaliano

Waziri wa Uingereza anayesimamia mchakato wa nchi hiyo kujitoa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama BREXIT ametangaza kuwa nchi yake iko tayari kujitoa katika umoja huo bila kufikiwa mwafaka kamili.

Michael Gove ameyasema hayo leo alipozungumzia kikao cha karibuni cha wakuu wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya ambacho katika taarifa ya ufungaji wake kilisema Uingereza ndiyo inayobeba jukumu la kuyatoa kwenye mkwamo mazungumzo ya Brexit ambayo yamekwama hivi sasa; na akabainisha kuwa: Kwa sasa, mwafaka hautapatikana kuhusu biashara huru na maamuzi yaliyochukuliwa na wakuu wa nchi wanachama wa EU yametamatisha mazungumzo hayo kuhusiana na biashara.

Uingereza ilijitoa rasmi katika Umoja wa Ulaya Januari 31, 2020 lakini itaendelea kufuata kanuni za umoja huo hadi mwisho wa mwaka huu kwa kufuata kile kilichoelezwa kama utaratibu wa kipindi cha mpito.

Tofauti na hitilafu kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit zingaliko pale pale.

Majadiliano kuhusu namna uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Uingereza utakavyokuwa baada ya kumalizika kipindi hicho yamekwamisha mazungumzo kati ya Brussels na London na kuiweka mashakani hatima ya Brexit.../