Watu wanaofariki dunia kwa Covid-19 barani Ulaya wanazidi kuongezeka
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na maambukizi ya virusi vya corona barani Ulaya imefika zaidi ya 250,000 licha ya kutekelezwa vizuizihatua mbalimbali za kudhibiti maambukizi.
Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kuwa, takwimu mpya zinaonyesha kuwa idadi ya watu walioaga dunia kwa maradhi ya Covid-19 barani Ulaya imefikia zaidi ya 250,000. Watu milioni 7 na 366,028 wamepatwa na ugonjwa wa Covid-19 barani humo.
Katika wiki ya karibuni kwa mara ya tatu Italia imeshadidisha hatua za kudhibiti maambukizi ya corona nchini humo. Jeremy Farrar Mshauri wa Masuala ya Sayansi wa Serikali ya Uingereza pia amesema kuwa ni lazima kutekelezwa karantini ya haraka iwezekanavyo nchini kote kwa muda wa wiki tatu ili kudhibiti maambukizi ya corona.
Hadi sasa watu 741,212 wameambukizwa corona nchini Uingereza kufuatia kuongeza mamabukizi elfu 18 na 804 hiyo jana. Aidha watu zaidi ya elfu 43 wameaga dunia kwa maradhi ya Covid-19 nchini humo.
Wakati huo huo viongozi wa serikali ya Slovenia na Romania pia wameshadidisha utekelezaji wa karantini katika nchi hizo kufuatia kuongeza kesi mpya za maambukizi ya corona. Slovenia tayari imetangaza hali ya hatari nchini humo kwa muda wa siku 30 tangu jana kutokana na kushtadi maambukizi ya corona. Kwa mujibu wa takwimu za serikali, katika muda wa saa 24 zilizopita watu elfu nne wamethibitika kuambukizwa corona huko Romania nchi ambayo ina jamii ya watu milioni 20.