Waislamu Waanza kusherehekea Maulidi ya Mtume Muhammad na Wiki ya Umoja
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64298
Leo tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu, inasadifia na siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (saw) na kuanza Wiki ya Umoja baina ya Waislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 29, 2020 02:55 UTC
  • Waislamu Waanza kusherehekea Maulidi ya Mtume Muhammad na Wiki ya Umoja

Leo tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu, inasadifia na siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (saw) na kuanza Wiki ya Umoja baina ya Waislamu.

Wanazuoni wengi wa madhehebu ya Ahlusunna wanasema kuwa Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal Mwaka wa Tembo katika mji mtakatifu wa Makka. 

Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya Umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Japokuwa Waislamu wa madhehebu mbalimbali wanahitilafiana katika baadhi ya mitazamo ya kisheria (fiqhi) na kadhalika, lakini wote  wanashirikiana katika mambo mengi ya msingi kama kumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja, kitabu kitakatifu cha Qur'ani, Siku ya Kiyama, Utume wa Nabii wa Mwisho, Muhammad (saw) na kadhalika. 

Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole (18 December 1854 – 29 December 1931) ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na kila mtu aliyemuona, na kwamba yeye binafsi hajawahi kuona wala hatamuona tena na kusikia mwanadamu mwingine mithili yake.

Sherehe za Maulidi na kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) mwaka huu zinaandamana na huzuni na majonzi makubwa ya Waislamu kote duniani kutokana na kitendo cha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na jarida la Charlie Hebdo la nchi hiyo la kumtusi na kumvunjia heshima Mtume huyo ambaye Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni rehma kwa walimwengu wote. 

Kwa mnasaba wa tukio hili adhimu la kuzaliwa mbora wa walimwengu, Idhaa ya Kiswahili Redio tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote dunia na kwa watetezi na wapenda haki popote pale walipo.