Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Venezuela
(last modified Sun, 20 Dec 2020 11:29:27 GMT )
Dec 20, 2020 11:29 UTC
  • Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Venezuela

Licha ya kufeli kwa sera za vikwazo za Marekani dhidi ya Venezuela, lakini viongozi wa Washington wangali wamekumbatia siasa hizo za mashinikizo na kuendelea kutekeleza siasa hizo zilizoshindwa na kugonga ukuta dhidi ya nchi hiyo ya Amerka ya Latini.

Katika uwanja huo, Wizara ya Hazina ya Marekani imetangaza kuiwekea vikwazo vipya Venezuela kwa kisingizio kufanyika udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hazina ya Marekani Ijumaa iliyopita ya tarehe 18 Desemba iliwajumuisha katika orodha yake ya vikwazo shakhsia wawili na asasi moja yenye mfungamano na serikali. Hatua hiyo inalenga kuishinikiza zaidi serikali halali ya Venezuela katika siku hizi za mwisho za uhai wa serikali ya Rais Donald Trump ambaye anapaswa kukabidhi madaraka mwezi ujao kwa Joe Biden baada ya kubwagwa vibaya katika uchaguzi wa mwezi uliopita.

Maafisa wa serikali ya Marekani wanadai kwamba, kumefanyika udanganyifu katika uchaguzi katika hali ambayo, ushindi mkubwa wa muungano wa rais Nicolas Maduro katika uchaguzi huo, unahesabiwa kuwa pigo jingine kwa siasa za Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Latin America.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

 

Marekani katika miaka ya hivi karibuni hususan miaka minne iliyopita imeshadidisha siasa za chuki, hasama na uingiliaji mambo ya ndani dhidi ya Venezuela na kumuweka katika mashinikizo makubwa kiongozi wa nchi hiyo Rais Nicolas Maduro. Ili kufikia malengo yake haramu, Marekani imetumia njia ya mbalimbali kama wenzo wa vikwazo vikubwa vya kiuchumi na kisiasa, kuwasaidia wapinzani wa ndani na kuwapatia himaya na misaada ya kifedha na kisiasa hususan Juan Guaido, kiongozi wa upinzani na hata kumtambua kama Rais wa Venezuela. Si hayo tu, Marekani imeunga mkono hata njama za mapinduzi bila kusahau uhaini na ushiriki wa Washington katika mipango ya uharibifu wa miundomsingi ya Venezuela kama vile kituo cha ugavi wa umeme.

Pamoja na njama zote hizo, lakini serikali ya Maduro ikipata himaya na uungaji mkono wa wananchi imeweza kulinda nfasi yake ya kisiasa nchini humo. Katika uwanja huo, ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa Bunge na kupata wingi wa viti chama tawala, ni ishara ya wazi ya kupendwa Maduro na wananchi wa Venezuela.

Hata hivyo, viongozi wa Marekani na wapinzani wa ndani wanaounga mkono siasa za Washington katika siku za hivi karibuni na licha ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa Bunge, lakini wanafanya kila wawezalo kuutia dosari uchaguzi huo kwa madai kwamba, kulifanyika udanganyifu katika zoezi hilo na hivyo kuupa changamoto ushindi wa wafuasi wa Rais Maduro.

Sergei Melik-Bagdasarov, balozi wa Russia nchini Venezuela anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba, hatua ya baadhi ya mataifa ya kukataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo, inabainisha kufeli kwao katika kukabiliana na ukweli wa mambo.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela anayeungwa mkono na Marekani

 

Hii ni katika hali ambayo, Rais Nicolas Maduro amefichua juu ya kutumika gharama ya mamilioni ya dola kwa ajili ya kuyaajiri makundi ya uhalifu ili yazushe vurugu na machafuko wakati wa uchaguzi, hatua ambazo zimefanyika kwa uongozi wa Rais wa Marekani Dolad Trump. Aidha Maduro ameeleza kwamba, Marekani ilitoa fedha hizo na kwa kushirikiana na Colombia, mataifa hayo mawili yaliandaa mipango ya kufanya hujuma dhidi ya mwenendo wa uchaguzi wa Bunge nchini Venezuela.

Uchaguzi wa Bunge nchini Venezuela ulikuwa na umuhimu sana katika uga wa siasa za nchi hiyo hasa katika kipindi cha sasa. Licha ya kufanya njama lukuki za Marekani na washirika wake zilizokuwa zikilenga kuuvuruga, lakini kwa kufanyika uchaguzi huo na kuibuka na ushindi chama tawala cha Maduro, kwa mara nyingine tena hilo limeimarisha nafasi ya kiongozi huyo baina ya wananchi na kusambaratisha siasa za chuki za serikali ya Washington dhidi ya Caracas.

Rais Donald Trump wa Marekani

 

Hii ni katika hali ambayo, kwa kuzingatia uchaguzi wa Marekani wa mwezi uliopita wa Novemba na fedheha kubwa iliyojitokeza baada ya uchaguzi huo, viongozi wa Washington hawana haki ya kutia dosari chaguzi za mataifa mengine.

Pamoja na hayo, viongozi wa Marekani wamepuuza na kufumbia macho kugonga ukuta siasa zao za huko nyuma na hivi sasa wanafanya kila wawezalo kushadidisha vikwazo dhidi ya serikali na taifa la Venezuela ili kwa njia hiyo labda wataweza japo kidogo kurejesha heshima na nafasi yao iliyopotea. Hata hivyo kwa kuzingatia mkondo wa mambo unavyokwenda pamoja na matukio ya kieneo na kimataifa ni jambo lililo mbali kwa viongozi wa Marekani kuweza kufanikiwa katika hilo.

Tags