Russia: Iran iko mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65799-russia_iran_iko_mstari_wa_mbele_katika_kupambana_na_ugaidi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametupilia mbali madai ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ya kuihusisha Iran na Al Qaeda; na akasema, kwa mujibu wa ushahidi uliopo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe ni mhanga wa ugaidi na iko mstari wa mbele pia katika kupambana kwa dhati na makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 16, 2021 13:08 UTC
  • Russia: Iran iko mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametupilia mbali madai ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ya kuihusisha Iran na Al Qaeda; na akasema, kwa mujibu wa ushahidi uliopo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe ni mhanga wa ugaidi na iko mstari wa mbele pia katika kupambana kwa dhati na makundi ya kigaidi.

Maria Zakharova ameyasema hayo leo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na akaongeza kuwa, si tu hakuna taarifa zozote zinazoashiria uwezekano wa kuwepo uhusiano kati ya Tehran na kundi hilo (Al Qaeda), lakini pia Iran yenyewe ni nchi ya kweli na yenye nia ya dhati katika suala la kupambana na ugaidi.

Zakharova amebainisha kuwa, kuna ushahidi mwingi unaothibitisha jinsi Iran inavyopambana kwa dhati na kwa juhudi kubwa na magaidi, mfano ukiwa ni katika nchi za Syria na Iraq.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia amesema, viongozi wa Marekani wananyamazia kimya ushahidi kuhusu mapambano athirifu ya Iran dhidi ya magaidi; na mwenendo huo unatokana na mtazamo wao mbaya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Pompeo

Hivi karibuni, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alidai kuwa, Iran ilitoa msaada katika upangaji wa mashambulio ya Septemba 11 na kwamba mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda umepata makao mengine mapya ambayo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Alipoulizwa na mwandishi wa habari wa IRNA kuhusu matarajio ya baadaye katika ustawi wa uhusiano wa Iran na Russia katika mwaka huu wa 2021, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia amesema, uhusiano wa Iran na Russia unaendelea kustawi katika nyuga mbalimbali  na kwamba uhusiano huo umesimama juu ya msingi wa ujirani mwema na kuheshimiana baina ya pande mbili; na nchi zote mbili zina azma ya kupanua na kustawisha mashirikiano na maelewano katika nyanja mbalimbali.../