Balozi wa Iran UN: Rais wa Marekani achukue hatua ya kwanza
(last modified Tue, 26 Jan 2021 07:35:01 GMT )
Jan 26, 2021 07:35 UTC
  • Balozi wa Iran UN: Rais wa Marekani achukue hatua ya kwanza

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu haina mpango wowote wa kufanya mazungumzo na Rais mpya wa Marekani Joe Biden, lakini inasubiri serikali mpya ya Washington ichukue hatua ya kwanza ya kuliondolea taifa hili vikwazo na kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Majid Takht Ravanchi alisema hayo jana Jumatatu katika mahojiano yake ya kwanza na shirika la habari la NBC News tangu Biden aapishwe na kuongeza kuwa, "mpira uko katika uwanja wa Marekani."

Akijibu swali la mwandishi wa habari wa NBC News, Richard Enge kuhusu iwapo Tehran imeshafanya mazungumzo na utawala wa Biden, Balozi Takht Ravanchi ameeleza bayana kuwa: Hapana! Hakuna mazungumzo yoyote yamefanyika kati ya Iran na Marekani tangu Biden achukue hatamu za uongozi.

Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haina mpango wowote wa kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja na Washington au yasiyo ya moja kwa moja kupitia serikali ya Uswisi. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, "ni juu ya Marekani kuamua hatua itakayochukua, sisi hatuna haraka."

Rais wa US, Joe Biden (kulia) na mtangulizi wake Donald Trump

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa, Biden anapaswa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za kugombea urais, ya kuirejesha Marekani katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA.

Ameongeza kuwa, maneno matupu hayatoshi, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuona serikali mpya ya Washington ikichukua hatua na kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.

 

Tags