EU na US kufanya mkutano wa kujaribu kuinusuru JCPOA
(last modified Fri, 29 Jan 2021 07:49:01 GMT )
Jan 29, 2021 07:49 UTC
  • EU na US kufanya mkutano wa kujaribu kuinusuru JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani amesema mazungumzo baina ya nchi za Ulaya na Marekani kuhusu kurejea Washington katika makubaliano ya nyuklia ya Iran yataanza hivi karibuni.

Heiko Mass amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Reuters na kuongeza kuwa, "iwapo Marekani itafanikiwa kurejea katika mapatano ya nyuklia ya Iran, hatua hiyo itapelekea kuondolewa vikwazo Iran sambamba na kuizuia Marekani isiiwekee Tehran vikwazo vipya."

Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani amedai kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kurejea katika majukumu yake na kutoendelea na hatua za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo.

Ikumbukwe kuwa, kutokana na nchi za Ulaya kuendeleza mwenendo wa kutotekeleza ahadi na majukumu yao katika JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo, tarehe Mosi Disemba 2020, bunge la Iran lilipitisha sheria yenye vipengele tisa iliyopewa jina la "hatua ya kistratejia ya kuondoa vikwazo na kulinda maslahi ya taifa la Iran".

Bendera za nchi zilizosalia katika maptano ya JCPOA baada ya US kujiondoa

Miongoni mwa vipengele vya sheria hiyo ni kulazimika serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20, kuongeza kiwango cha akiba ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha chini na kutakiwa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran liunde na kuanza kutumia mashinepewa za kizazi kipya aina ya M21R na 6IR.

Licha ya kuahidi kwa maneno, lakini Troika ya Ulaya inayoundwa na Ujerumani, Uingereza na Ufaransa imefeli kuidhaminia Iran maslahi yake ya kiuchumi kivitendo baada ya Marekani kujitoa kinyume cha sheria katika mapatano hayo tarehe 8 Mei mwaka 2018. 

 

 

Tags