EU: Diplomasia ichukue nafasi ya mashinikizo ya kiwango cha juu
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema 'diplomasia ya kiwango cha juu' inapaswa kuchukua nafasi ya 'mashinikizo ya kiwango cha juu.'
Josep Borrell amesema hayo kabla ya kuelekea Moscow na kufafanua kuwa, utawala wa sasa wa Marekani unapaswa kubadili mkondo kutoka ule wa vikwazo na mashinikizo ya juu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliokuwa ukitekelezwa na utawala wa Donald Trump na badala yake ukumbatie mazungumzo na diplomasia.
Borrell ameashiria uamuzi wa upande mmoja wa Trump wa kuiondoa Marekani katika mapatano hayo ya kimataifa na kueleza bayana kuwa: Sera ya mashinikizo imekuwa na matokeo hasi. Uongozi wa Joe Biden umeeleza wazi utayarifu wake wa kuirejesha Marekani katika JCPOA. Washirika wote wa JCPOA wapo tayari kwa hili.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa Washington iko tayari kurejea katika JCPOA, iwapo Tehran itafungamana kikamilifu na mapatano hayo.
Hii ni katika hali ambayo, Iran ilipunguza uwajibikaji wake katika JCPOA kwa kutumia kipengee cha 36 cha makubaliano hayo, kufuatia vitendo visivyo vya kimantiki vya Marekani na vilevile kushindwa madola ya Ulaya kufidia hasara ilizopata Iran baada ya Marekani kujiondoa.
Licha ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kukiri mara kadhaa kwamba Iran imeheshimu na kutekeleza kikamilifu ahadi na majukumu yake, mwaka 2018 serikali ya Marekani ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujitoa katika makubaliano ya pande kadhaa ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran.