Iran: Marekani ingali inakiuka azimio 2231 kwa vikwazo haramu
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Marekani inaendelea kukanyaga azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la umoja huo kwa kuliwekea taifa hili vikwazo kinyume cha sheria.
Majid Takht Ravanchi amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, utawala mpya wa Washington unadai kuwa unaunga mkono siasa jumuishi za pande kadhaa, lakini umekasirishwa na uamuzi wa ICJ.
Siku ya Jumatano, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) ilitoa hukumu ya kuiwajibisha Marekani kufuta mara moja vikwazo vyake vyote vinavyohusiana na masuala ya kibinadamu.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema kitendo cha utawala mpya wa Marekani kughadhabishwa na uamuzi huo wa mahakama ya kimataifa kinaashiria mwanzo ambao si mzuri.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameukosoa vikali utawala mpya wa Marekani unaoongozwa na Joe Biden kwa kuendelea kukiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN, la kutowekewa vikwazo taifa hili baada ya kufikia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Viongozi wa Iran wameutaja uamuzi huo wa ICJ kama ushindi mwingine kwa Jamhuri ya Kiislamu mkabala wa Marekani.