Mashambulio yatokanayo na chuki dhidi ya Uislamu yamekithiri nchini Ujerumani
Takwimu rasmi zilizotolewa nchini Ujerumani zinaonyesha kuwa, katika mwaka uliopita wa 2020 nchi hiyo ilishuhudia ongezeko kubwa la hujuma na mashambulio dhidi ya Waislamu na taasisi za Kiislamu.
Gazeti la kila wiki la Spiegel limeripoti kuwa, ukatili dhidi ya Waislamu unazidi kuongezeka nchini Ujerumani.
Takwimu zilizoripotiwa na gazeti hilo zinaonyesha kuwa, mnamo mwaka uliopita wa 2020 mashambulio na hujuma dhidi ya Waislamu na taasisi za Kiislamu zilikithiri, ambapo takriban kila siku yalitokea matukio mawili ya hujuma dhidi ya jamii hiyo.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani, matukio yasiyopungua 901 ya uhalifu yaliyofanywa dhidi ya Uislamu na Waislamu yalitokea mwaka 2020 nchini humo, likiwa ni ongezeko la asilimia mbili kulinganisha na mwaka wa kabla yake.

Matukio 884 ya uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Uislamu yaliripotiwa mwaka 2019 nchini Ujerumani. Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo imeeleza kuwa, akthari ya hujuma hizo zimefanywa na wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mpaka.
Ripoti rasmi zinaonyesha kuwa, katika mwaka uliopita wa 2020 yaliripotiwa matukio 77 ya kushambuliwa misikiti na maeneo ya kusalia ya Waislamu ambapo watu wapatao 48 walijeruhiwa pia katika hujuma na mashambulio hayo.
Waislamu nchini Ujerumani wameshabainisha mara kadhaa hofu na wasiwasi mkubwa walionao kutokana na vitendo vya uenezaji chuki dhidi ya Uislamu na hujuma zinazofanywa dhidi ya misikiti na vituo vyao vya kidini na kuomba zichukuliwe hatua kali za kiusalama za kulinda vituo hivyo.../