Mashirika 99 yataka kusitishwa mauzo ya silaha kwa Saudia, UAE
https://parstoday.ir/sw/news/world-i66804-mashirika_99_yataka_kusitishwa_mauzo_ya_silaha_kwa_saudia_uae
Mashirika 99 ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yametoa mwito wa kusitishwa mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu sambamba na kuondolewa mzingiro dhidi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 13, 2021 08:53 UTC
  • Mashirika 99 yataka kusitishwa mauzo ya silaha kwa Saudia, UAE

Mashirika 99 ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yametoa mwito wa kusitishwa mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu sambamba na kuondolewa mzingiro dhidi ya Yemen.

Katika taarifa ya pamoja ya jana Ijumaa, mashirika hayo yamesema asilimia 80 ya jamii ya Yemen wakiwemo watoto milioni 12 wanahitaji misaada ya dharura ya kibinadamu kutokana na uvamizi na mzingiro wa muungano wa kijeshi wa Saudia.

Mbali na kutoa mwito wa kusitishwa mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, mashirika hayo yametaka kusitishwa mara moja vita dhidi ya nchi hiyo maskini sambamba na kuondolewa mzingiro na kufunguliwa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Sana'a na Bandari ya Hudaydah ili misaada ya kibinadamu iweze kufikishwa katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.

Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Italia ilitangaza kubatilisha mikataba ya uuzaji wa mabomu na makombora kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Aidha Italia ilisema haitatoa tena vibali vipya vya kuziuzia silaha nchi hizo mbili.

Vita vya kidhulma vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen tokea Machi 2015 hadi sasa vimesababisha kuuliwa Wayemeni zaidi ya elfu 16, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine

Siku chache kabla ya tangazo hilo la Italia, serikali ya Joe Biden pia ilitagaza kusitisha uuzaji silaha za Marekani kwa Saudia na ndege za kivita aina ya F-35 kwa Imarati. Siku chache kabla ya Biden kuapishwa kuwa rais mpya wa Marekani, Donald Trump, aliyekuwa rais wa nchi hiyo aliafiki mpango wa kuiuzia Imarati ndege 50 za kivita aina ya F35 zenye thamani ya dola bilioni 23.

Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Italia ndio wauzaji wakubwa zaidi wa silaha barani Ulaya kwa Saudia Arabia. Marekani nayo ndiye muuzaji mkubwa zaidi wa silaha kwa Saudia Arabia katika miaka ya hivi karibuni.