UN yatoa mwito wa kuheshimiwa makubaliano ya JCPOA
Naibu Msemaji wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekaribisha hatua ya Marekani ya kumwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo ya kuondoa madai ya serikali iliyotangulia ya nchi hiyo kuhusu kurejeshwa vikwazo vyote vya UN dhidi ya Iran.
Farhan Haq amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa unataka pande zote husika kuheshimu na kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Amesema UN inatumai kuwa, hatua zitakazochukuliwa katika siku na wiki zijazo zitahakikisha kuwa washiriki wote wa mapatano hayo ya kimataifa wanafungamana nayo kikamilifu.
Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, JCPOA ni mafaniklio makubwa ya kidiplomasia ambayo yanapaswa kulindwa na kuheshimiwa.
Jana Ijumaa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema hatua ya Washington ya kuliandikia barua Baraza la Usalama ya kutaka kufutwa madai ya serikali iliyopita ya Donald Trump kuhusu kurejeshwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran inakusudia kuimarisha nafasi ya US katika miamala yake na taasisi hiyo ya UN juu ya Iran.
Iran inasisitiza kwamba, kwa kuzingatia kuwa ni Marekani ndiyo ilijitoa katika mapatano hayo na kuwa hatua ya Iran ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo ilikuwa hatua ya kawaida na ya kisheria katika kukabiliana na hatua hiyo ya Marekani, hivyo ni wazi kuwa itarejea katika mapatano hayo iwapo tu itaondolewa vikwazo vyote vinavyotekelezwa dhidi yake kinyume cha sheria.