Umoja wa Ulaya wakerwa na usimamishwaji wa protokali ziada ya NPT
https://parstoday.ir/sw/news/world-i67276-umoja_wa_ulaya_wakerwa_na_usimamishwaji_wa_protokali_ziada_ya_npt
Umoja wa Ulaya umetoa taarifa ukibainisha kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuanza kutekeleza sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) kwa ajili ya kusimamisha utekelezaji wa protokali ziada ya mkataba wa NPT.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2021 04:20 UTC
  • Umoja wa Ulaya wakerwa na usimamishwaji wa protokali ziada ya NPT

Umoja wa Ulaya umetoa taarifa ukibainisha kutoridhishwa kwake na uamuzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuanza kutekeleza sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) kwa ajili ya kusimamisha utekelezaji wa protokali ziada ya mkataba wa NPT.

Umoja huo umedai katika taarifa hiyo kwamba unaendelea kuheshimu mapatano ya kimataifa yaliyofikiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi sita kubwa za dunia mashuhuri kama JCPOA na kusisitiza kuwa utaendelea kuyaunga mkono mapatano hayo katika mazingira nyeti ya hivi sasa.

Taarifa hiyo imetolewa katika hali ambayo tayari Iran ilikuwa imeuonya Umoja wa Ulaya kuhusiana na nchi tatu za Ulaya mashuhuri kama Troika kutotekeleza wajibu wao kuhusiana na mapatano hayo lakini zikawa zimepuuza onyo hilo.

Taarifa hiyo imeendelea kudai kuwa usimamishwaji wa pritokali ziada utapunguza pakubwa uwezo wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA wa kuendelea kusimamia miradi ya nyuklia ya Iran na kuhakikisha kuwa inatumika tu kwa malengo ya amani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, usimamishaji wa protokali ziada una maana kwamba sasa IAEA haitakuwa tena na uwezo mkubwa wa kupata taarifa kamili za miradi ya nyuklia ya Iran na hasa kuhusiana na urutubishaji wake wa madini ya urani.

Mfumo wa Instex ambao haukutekelezwa na Umoja wa Ulaya

Kufuatia hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na Marekani mnamo Mei 8, 2018, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Iran ilifanya juhudi kubwa za kulinda mapatano ya JCPOA kwa sharti kwamba pande nyingine za mapatano hayo nazo zitekeleze majukumu yao lakini pande hizo na hasa nchi za Ulaya hazikuchukua hatua yoyote ya kutekeleza ahadi zao za mapatano hayo.

kwa msingi huo Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran tarehe 8, Mei 2019, lilitangaza kuwa Iran nayo ingeanza kupunguza hatua kwa hatua uwajibikaji wake kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya mapatano hayo ya JCPOA, ili kulinda haki na maslahi yake ya kitaifa.

Kwa msingi huo Iran ilichukua hatua ya kusimamisha protokali ziada mnamo tareje 23 ya mwezi huu wa Februari.

Kwa mujibu wa vipenge vilivyotajwa, Iran ina haki ya kusimamisha utekelezaji wa ahadi zake zote au baadhi ya ahadi hizo iwapo itahisi kuwa pande nyingine za mapatano hayo hazitekelezi ahadi zao ipaswavyo.