Waingereza waendelea kuandamana, wapinga ukatili wa kijinsia
(last modified Tue, 16 Mar 2021 09:25:42 GMT )
Mar 16, 2021 09:25 UTC
  • Waingereza waendelea kuandamana, wapinga ukatili wa kijinsia

Mamia ya wananchi wa Uingereza wameendelea kuandamana katika mitaa ya kandokando ya Bunge la nchi hiyo wakipinga mauaji yaliyofanywa na afisa wa polisi dhidi ya Sarah Everard, mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 33. Waandamanaji hao wamefunga kabisa barabara za kandokando ya Bunge la nchi hiyo.

Baadhi ya waandamanaji hao wameanzisha mgomo wa kuketi chini mbele ya jengo la polisi ya London lililoko karibu na majengo ya Bunge na ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, huku wakipiga nara zinazopinga ukatili dhidi ya wanawake na kutokuwepo usawa wa kijamii. Polisi ya Uingereza imewatia nguvuni waandamanaji kadhaa. 

Jumatatu ya jana Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Priti Patel alisema serikali imejifunza kutokana na tukio la Jumamosi iliyopita na kwamba itafanya juhudi za kurejesha imani ya wananchi na kuzidisha usalama wa wanawake mitaani.

Sambamba na hayo Bunge la Uingereza limeanzisha mikakati ya kuongeza uwezo na madaraka ya polisi ya kukandamiza maandamano ya raia. 

Mauaji yaliyofanywa na afisa wa polisi ya Uingereza dhidi ya mwanamke, Sarah Everard aliyekuwa njiani akirejea nyumbani siku ya tarehe 3 mwezi huu wa Machi huko kusini mwa London yameishtua jamii ya nchi hiyo na kusababisha malalamiko makubwa nchini humo dhidi ya ukatili wa maafia wa polisi na unyanyasaji dhidi ya wanawake.   

Tags