Mwana wa Trump amfanyia istihzai rais wa Marekani, Joe Biden
Mwana wa kiume wa rais wa zamani wa Marekani, amerusha katika mtandao wa Twitter kipande cha video kilichotengenezwa maalumu kwa ajili ya kumfanyia istihzai Joe Biden baada ya rais huyo wa Marekani kula mweleka mara tatu mfululizo wakati alipokuwa anapanda ngazi ya ndege.
Shirika la habari la FARS limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Donald Trump Junior, mwana wa kiume wa rais wa zamani wa Marekani, Ijumaa alisambaza video hiyo katika ukurasa wake wa Twitter inayomuonesha Joe Biden akianguka na kula mweleka mfululizo wakati alipokuwa anapanda ngazi za ndege na pembani mwake ndani ya video hiyo amemuweka baba yake yaani Donald Trump akicheza Golf.
Kula mweleka mfululizo Biden wakati akipanda ngazi ya ndege ya Rais huko Marekani kunaendelea kufanyiwa istihzai za kila namna katika mitandao ya kijamii huku watu wengi wakisema kwamba huenda Biden anahitaji kiti kikubwa zaidi cha kupandia ngazi. Wengine wamesema, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aanze kufanya mazoezi ya kula kiapo cha kuwa rais wa nchi hiyo.
Juzi Ijumaa, Rais Joe Biden wa Marekani alitelea na kuanguka mara tatu mfululizo wakati alipokuwa anapanda ngazi ya ndege, na hivyo kushadidisha uvumi kwamba hayuko salama hata kidogo kiafya.
Akiwa na umri wa miaka 78, Biden ndiye rais kizee zaidi kuwahi kuingia madarakani huko Marekani. Rais huyo alikuwa anakwenda kuonana na jamii ya Wamarekani wenye asili ya Asia.
Kabla ya hapo pia, yaani mwezi Novemba 2020, mguu wa Joe Biden ulipata majeraha wakati alipokuwa akicheza na mbwa, na alipitisha wiki kadhaa kabla ya kupona.