Watoto wanaotafuta hifadhi kupelekwa katika kambi za kijeshi jimboni Texas
https://parstoday.ir/sw/news/world-i68290-watoto_wanaotafuta_hifadhi_kupelekwa_katika_kambi_za_kijeshi_jimboni_texas
Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imeafiki kupelekwa maelfu ya watoto wanaotafuta hifadhi katika kambi za kijeshi jimboni Texas kufuatia hali ya mgogoro iliyojitokeza katika mpaka wa kusini wa Marekani. Watoto hao wanatazamiwa kupelekwa katika kambi mbili za kijeshi bila ya wazazi wao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2021 06:51 UTC
  • Watoto wanaotafuta hifadhi kupelekwa katika kambi za kijeshi jimboni Texas

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imeafiki kupelekwa maelfu ya watoto wanaotafuta hifadhi katika kambi za kijeshi jimboni Texas kufuatia hali ya mgogoro iliyojitokeza katika mpaka wa kusini wa Marekani. Watoto hao wanatazamiwa kupelekwa katika kambi mbili za kijeshi bila ya wazazi wao.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani John Kirby amesema jeshi la nchi hiyo limekubali ombi la Idara ya Afya na Huduma za Kibinadamu (HHS) iliyotaka watoto hao wanaotafuta hifadhi nchini Marekani wenye umri wa chini ya miaka 18 kupewa makazi ya muda kwenye kambi hizo za kijeshi.  

John Kirby, Msemaji wa Pentagon 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto hao wanaotafua hifadhi ambao wako peke yao bila ya wazazi wao wanatazamiwa kupelekwa katika kambi ya jeshi la anga ya Lockland katika kituo cha San Antonio na kwenye kambi ya Fort Bliss katika jimbo la Texas. 

Wizara ya Afya na Tiba ya Marekani imeomba kuwa, watoto elfu tano wapelekwe katika kambi ya jeshi ya Fort Bliss na wengine 300 wapewe hifadhi katika kambi ya Lockland lakini hadi sasa bado haijafahamika iwapo Pentagon imeafiki ombi hilo au la. 

Zaidi ya mabarobaro elfu 15 na 500 wanaotafuta hifadhi wanashikiliwa katika mahabusu za askari walinda mipaka wa Marekani. Mabarobaro hao wapo katika hali isiyoridhisha. 

Rais Joe Biden wa Marekani ambaye baada ya kushika hatamu za uongozi alidhihirisha kasi ya kuachana na siasa za  Trump za kukabiliana vikali na wahajiri, hivi sasa amepuuza ahadi alizotoa huko nyuma kuhusu suala hilo kwa kisingizio cha maambukizi ya corona akisema kuwa sasa si muda mwafaka kwa wanaotafuta hifadhi kuingia Marekani.