Mgogoro katika uhusiano wa Russia na Marekani
Balozi wa Russia nchini Marekani amesema kuwa licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na Moscow kwa ajili ya kuanzishwa mazungumzo na Washington lakini bado uhusiano wa nchi mbili hizo uko katika mgogoro mkubwa.
Akibainisha suala hilo hapo jana Jumatano, Balozi Anatoly Antonov amesema kuwa licha ya juhudi kubwa ambazo zimefanywa na serikali ya Moscow kwa madhumuni ya kuanzisha mazungumzo ya kivitendo kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili lakini juhudi hizo hazijakuwa na mafanikio yoyote.
Anatoly Antonov amesema kwamba Washington daima inaharibu misingi muhimu ya uhusiano huo ambao haukujengwa kirahisi, na kuwa haijakoma kuitishia Russia na vilevile kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.
Balozi wa Russia mjini Washington ametoa mfano katika uwanja huo na kueleza kuwa katika mwaka uliopita wa 2020 pekee na licha ya kuwepo janga la corona, lakini Marekani iliiwekea Russia vikwazo zaidi ya mara 10 na kwamba tokea mwaka 2011 hadi sasa imeiwekea nchi hiyo vikwazo zaidi ya mara 93.
Anatoly Antonov, amesema zaidi ya Warussia 350 na mashirika 500 ya nchi hiyo yanakabiliwa na vikwazo vya kiuadui vya Marekani na kuwa Congress ya Marekani nayo haijasitisha vitendo vyake vya uhasama dhidi ya serikali ya Moscow, ambapo katika miaka ya karibuni bunge hilo limetunga na kupitisha sheria 10 za kuiadhibu Russia. Hii ni pamoja na kuwa kuna miswada mingine 15 katika bunge hilo inayosubiri kupitishwa dhidi ya Moscow.