Makumi wafariki dunia kutokana na mafuriko, maporomoko ya ardhi Indonesia
Makumi ya watu wamepoteza maisha na wengine wengi hawajulikani walipo baada ya kutokea mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Indonesia.
Duru za habari zinasema kuwa, mbali na watu zaidi ya 44 kuaga dunia, wengine wengi hawajulikani walipo baada ya kutokea mafuriko na maporomoka ya udongo alfajiri ya leo katika kisiwa cha Flores mashariki mwa Indonesia.
Msemaji wa Idara ya Kupambana na Majanga ya Indonesia, Raditya Jati ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mabwawa katika wilaya ndogo nne za eneo hilo yamevunja kingo zake, ambapo maji yake yamesomba nyumba zaidi ya 10,000.
Mbali na kisiwa hicho, mafuriko makubwa yameripotiwa pia katika jiji la Bima, katika mkoa jirani wa Nusa Tenggara Magharibi. Televisheni za Indonesia zimeonesha mamia ya watu wakiokolewa na maafisa usalama na kupelekwa maeneo salama.

Baadhi ya waokoaji wameonekana wakibeba miili ya watu waliofariki dunia. Magari ya wagonjwa na ya kawaida yameonekana yakipita na wahanga wa maafa hayo katika barabara zilizojaa matope kuwawahisha mahospitalini.
Mafuriko na maporomoko ya ardhi hushuhudiwa mara kwa mara nchini Indonesia hususan katika misimu ya mvua za masika. Mapema mwaka huu, watu zaidi ya 40 waliaga dunia kutokana na mafuriko mengine yaliyoshuhudiwa katika mji wa Sumedang, mkoa wa Java Magharibi.