Mpango wa Marekani kununua maji mazito ya Iran unaiva
Vyombo vya habari vya Marekani vimesema mpango wa serikali ya Washington kununua maji mazito ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeingia katika hatua yake ya mwisho.
Ernest Moniz. Waziri wa Nishati wa Marekani amesema mazungumzo juu ya muamala huo wa kibiashara kati ya Tehran na Washington yanaelekea kutamatika. Akiongea katika warsha juu ya sera za nchi hiyo iliyoandaliwa na shirika la Politico jana Jumatano, Waziri wa Nishati wa Marekani alisema kama tunavyonukuu: "Kwa sasa tumejikita juu ya kutekeleza awamu ya kwanza ya kununua maji hayo mazito ya Iran." Mwisho wa kunukuu.
Serikali ya Washington hivi karibuni ilitangaza azma yake ya kununua maji mazito ya nyuklia ya Iran kwa dola milioni 8.6 za Marekani. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa inatarajia kuwa tani 32 za maji mazito kutoka Iran zitakabidhiwa kwa nchi hiyo karibuni hivi. Washington imesema maji hayo mazito yatakidhi haja ya ndani ya Marekani kwa ajili ya viwanda na utafiti. Habari ya Iran kuiuzia Marekani makumi ya tani za maji mazito ya nyuklia pia imethibitishwa na maafisa husika hapa nchini kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1. Hii ni katika hali ambayo, Russia nayo inapanga kununua tani 40 za maji mazito ya Iran.
Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran hivi karibuni alinukuliwa na waandishi wa habari akisema kuwa, baada ya Russia na Marekani, yumkini madola mengine makubwa yakaagiza maji mazito ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.