Wasiwasi wa Pakistan wa kuweko magenge ya kigaidi nchni Afghanistan
(last modified Mon, 27 Sep 2021 04:32:11 GMT )
Sep 27, 2021 04:32 UTC
  • Wasiwasi wa Pakistan wa kuweko magenge ya kigaidi nchni Afghanistan

Waziri Mkuu wa Pakistan ameelezea wasiwasi wake kutokana na kuweko magenge ya kigaidi katika nchi jirani ya Afghanistan kama vile Daesh (ISIS) na Tehrik-i-Taliban.

Imran Khan amesema hayo katika mahojiano na jarida la kila wiki la Newsweek la nchini Marekani na kuongeza kuwa, malengo ya magenge ya kigaidi nchini Afghanistan ni kuvuruga usalama na utulivu wa nchi hiyo iliyoathiriwa vibaya na vita.

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema, baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka, na madaraka ya Afghanistan kutwaliwa na kundi la Taliban hapo tarehe 15 Agosti, kulipatikana matumaini kwamba usalama na amani itaenea kote nchini humo na kutakuwa na manufaa mazuri kwa Pakistan na nchi za ukanda huu.

Amma katika juhudi zake za kuhalalisha ushirikiano wa serikali yake na serikali ya mpito ya Taliban huko Afghanistan, Imran Khan amesema, Islamabad inafanya juhudi za kupambana na magenge ya kigaidi ndani ya ardhi ya Afghanistan.

Matamshi ya Waziri Mkuu wa Pakistan kuhusu wasiwasi wake wa kuweko magenge ya kigaidi nchini Afghanistan  wakiwemo Madaesh na Tehrik-i-Taliban yanatokana na daghadagha na hofu ya serikali ya Pakistan ya kujipenyeza magaidi hao katika ardhi ya nchi hiyo kutokea Afghanistan.

Magaidi wa Daesh (ISIS)

 

Katika miaka ya hivi karibuni, Daesh na Tehrik-i-Taliban yalikuwa ni miongoni mwa magenge yenye misimamo mikali ya kigaidi ambayo yalihatarisha usalama na utulivu wa Pakistan. Katika hali ambayo kuanzia tarehe 15 Agosti hadi hivi sasa, Afghanistan imo mikononi mwa kundi la Taliban, viongozi wa Pakistan wana matumaini kundi hilo litazingatia zaidi wasiwasi wa viongozi hao kuhusu usalama wa Pakistan na litapambana vikali na vilivyo na magaidi wa Daesh na Tehrik-i-Taliban ili kuzuia wasiingie katika ardhi ya Pakistan kutokea Afghanistan.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na kabla ya kundi la Taliban kuudhibiti tena mji wa Kabul, muda wote Pakistan na Afghanistan zilikuwa zinatuhumiwa kuwa hazipambani ipasavyo na magenge ya kigaidi bali baadhi ya wakati zilikuwa zinashutumiana kuyaunga mkono magenge hayo.

Kwa kuzingatia maneno yanayosema kuwa Pakistan ni msihrika wa kisiasa wa kundi la Taliban katika serikali yao huko Afghanistan, viongozi wa Islamabad sasa wanataka kundi la Taliban lichukue hatua ambazo zitaondoa wasiwasi wa Pakistan wa kujipenyeza nchini humo magenge ya kigaidi kutokea Afghanistan. Inaonekana wazi kwamba hofu ya viongozi wa Islamabad itapungua kama kundi la Taliban litapambana na magenge ya ISIS na Tehrik-i-Taliban ambayo katika miaka ya huko nyuma yamesababisha maafa ya kila namna ndani ya Pakistan.

Magaidi wa Tehrik-i-Taliban

 

Hivi sasa kundi la Taliban linapigania uungaji mkono wa kidiplomasia na kukubalika kimataifa. Sasa kama litaweza kupambana na magenge hayo mawili ya ISIS na Tehrik-i-Taliban na kuzuia yasijipenyeze Pakistan, bila ya shaka yoyote halitakosa uungaji mkono wa kidiplomasia wa Islamabad.

Kundi la Taliban linalazimika kuithibitishia dunia kivitendo kuwa silo tena lile kundi la kigaidi la miaka 20 iliyopita hasa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa serikali ya Rais Ashraf Ghani iliyopinduliwa na kundi la Taliban ndiyo bado inayotambuliwa rasmi kimataifa. Sasa ili liweze kuchukua nafasi ya kutambuliwa rasmi kimataifa na kukubalika kuwa ni serikali halali, kundi la Taliban lina wajibu wa kuondoa wasiwasi uliopo ulimwenguni ukiwemo wa nchi zinazopakana na Afghanistan kama vile Pakistan.

Ikumbukwe pia kuwa, miaka 20 iliyopita, wakati kundi la Taliban lilipotwaa madaraka nchini Afghanistan, Pakistan ilikuwa moja ya nchi tatu tu duniani zilizotambua utawala wa Taliban huko Afghanistan, na ni Pakistan hiyo hiyo ndiyo iliyotoa mchango mkubwa wa kupinduliwa serikali ya Taliban miaka 20 iliyopita,

Wachambuzi wa mambo wanasema, hivi sasa kundi la Taliban halitodharau wasiwasi huo wa viongozi wa Pakistan na inatarajiwa watachukua hatua za kupambana na magenge ya kigaidi hasa Daesh na Tehrik-i-Taliban ili kupunguza daghadagha na wasiwasi wa viongozi wa Islamabad.