Mtetemeko wa ardhi waua makumi ya watu nchini Pakistan
Mtetemeko wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 5.9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea mapema jana katika mkoa wa Baluchistan, kusini magharibi mwa Pakistan na kuua watu wasiopungua 23.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Pakistan, mbali na makumi ya watu kuaga dunia katika zilzala hiyo, mamia ya wengine wamejeruhiwa, huku maelfu ya wengine wakiachwa bila makazi.
Suhail Anwar Shaheen, Naibu Kamishna wa serikali katika eneo hilo amesema juhudi za uokoaji na kutafuta miili ya waliofariki katika tukio hilo la kimaumbile zingali zinaendelea.
Amesema kitovu cha zilzala hiyo kilikuwa karibu na mji wa Harnai, yapata kilomita 15 kaskazini mashariki mwa mkoa wa Baluchistan.
Afisa huyo wa serikali katika eneo hilo amesema yumkini idadi ya vifo vya mtetemeko huo wa ardhi ikaongezeka, kutokana na idadi kubwa ya migodi ya mkaa katika mji wa Quetta, makao makuu ya mkoa huo.

Shaheen amesema wanahofia kuwa wachimba migodi wengi wamefukiwa ardhini baada ya kujiri mtetemeko huo, kwani aghalabu yao walikuwa tayari wameshaingia kazini.
Mkoa wa Baluchistan ulioko kusini magharibi mwa Pakistan umekuwa ukishuhudia mitetemeko ya ardhi ya mara ya kwa mara, lakini tetemeko lililoitikisa nchi hiyo, ni lile la mwaka 1935, lililoua watu 35,000.