Kukosoa Uturuki utendaji wa Umoja wa Ulaya ulio dhidi ya Uislamu
(last modified Thu, 04 Nov 2021 23:53:26 GMT )
Nov 04, 2021 23:53 UTC
  • Kukosoa Uturuki utendaji wa Umoja wa Ulaya ulio dhidi ya Uislamu

Ukosoaji mtawalia wa viongozi wa Uturuki dhidi ya Umoja wa Ulaya hususan sera za chuki dhidi ya Uislamu za umoja huo, zinapaswa kutathminiwa kama juhudi za Ankara za kukabiliana na sera za madola ya Magharibi dhidi ya serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan na kuimarisha wenzo wa kuishinikiza jumuiya hiyo ya Ulaya.

Kufuatia kukwama huko viongozi wa serikali ya Uturuki hususan Rais Erdogan mwenyewe kabla ya hapo mara kadhaa ameutaka Umoja wa Ulaya utangaze wazi na bayana kama una nia au hauna azma ya kuipatia Uturuki uanachama wa umoja huo. Kuhusiana na hilo, Ibrahim Kalin, msemaji wa ikulu ya Rais wa Uturuki amekosoa vikali utendaji ulio wa chuki dhidi ya Uislamu wa madola ya Ulaya na Magharibi. Akizungumza na wanachuo wa mataifa ya Ulaya wanaoishi nchini Uturuki, Ibrahim Kalin amesema: Umoja wa Ulaya hauwezi kujijengea mustakabali mwema na mzuri kwa kupambana na dini tukufu ya Kiislamu. Na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana mwenendo wa kuuweka kando Uislamu na Waislamu unaofanywa na madola ya Magharibi na Ulaya unapaswa kuhitimishwa.

Ibrahim Kalin, msemaji wa ikulu ya Rais wa Uturuki

 

Msemaji wa ikulu ya Rais wa Uturuki kadhalika amesema bayana kwamba, Ulaya kwa upande mmoja inazungumzia suala la elimu, akili, kuweka wazi mambo, fikra na muelekeo wa staarabu kadhaa, lakini kwa upande wa pili inawafukuza watu wa jamii fulani kutokana na itikadi zao, mtindo wao wa maisha  au chimbuko la kaumu hiyo.

Matamshi ya afisa huyo wa ngazi za juu katika serikali ya Uturuki yanapaswa kutathminiwa katika fremu ya juhudi za viongozi wa Ankara za kujiunga na Umoja wa Ulaya. Ukweli wa mambo ni kuwa, matamshi haya maana yake ni kuwa, viongzoi wa Uturuki licha ya kuwa na mivutano ya mara kwa mara na baadhi ya madola ya Ulaya na chokochoko katika maeneo mbalimbali ya dunia, wangali wana matarajio ya kufunguliwa njia nchi hiyo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Kuhusiana na hili tunapaswa kusema kuwa, labda hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi rasmi wa Uturuki kuzungumzia wazi namna hii vizingiti vinavyoikabili nchi hiyo kwa ajili ya kukubaliwa uanachama katika Umoja wa Ulaya. Kabla ya hapo, duru za kisiasa na weledi wengi wa masuala ya kisiasa wa Uturuki na wa eneo hili, walikuwa wakiutambuulisha Umoja wa Ulaya kama klabu ya Wakristo. Lakini hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi rasmi wa serikali ya Ankara kuzungumzia wazi na bayana kabisa upande wa ubaguzi wa kidini wa Umoja wa Ulaya na kuendelea mchakato wa kujiunga nchi hiyo na umoja huo.

 Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

 

Licha ya kuwa viongozi wa Uturuki hawakiri wazi kuhusiana na jambo hili, lakini ukweli ambao haupaswi kufumbiwa macho ni huu kwamba, katika kipindi cha miongo sita iliyopita, Umoja wa Ulaya umekuwa ukikwepa kuipatia Uturuki uanachama katika uumoja huo ukichelea sababu mbalimbali kama tofauti za kidini, idadi kubwa ya watu na msukumo mkubwa wa Uturuki wa kuwa na taathira kwa mataifa ya Magharibi.

Fauka ya hayo, Umoja wa Ulaya una sababu nyingine za kutoikubalia hadi sasa Uturuki uanachama katika umoja huo ambazo ni sababu za kijeshi na kisiasa. Kwa mfano, Uturuki ni mwanachama wa Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi NATO, lakini haitoi ushirikiano kwa jumuiya hiyo ya kijeshi katika masuala ya Syria na Iraq.

Viongozi wa Uturuki wanaamini kuwa, Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi NATO, ambayo inahesabiwa kama msuli na nguvu ya kijeshi ya Marekani, itashirikiana na Uturuki pale tu viongozi wa Ankara wanakapofuata kibubusa na bila kuwahoji chochote maafisa na viongozi wa jumuiya hiyo hususan wa Marekani.

Alaa kulli haal, viongozi wa Umoja wa Ulaya wameitangazia na kuiainishia Uturuki vigezo maalumu ambapo kama itatekeleza basi inaweza kukubaliwa uanachama katika jumuiya hiyo kubwa zaidi barani Ulaya.

 

Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya ambaye mwezi huu alifanya safari mjini Athens kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za kumbukumbu ya mwaka wa 40 wa kujiunga Ugiriki na Umoja wa Ulaya aliisisitizia Uturuki kwamba: Endapo itaendelea kupuuza vigezo na maslahi ya umoja huo basi kuiadhibu na kutumia hatua za kujikinga dhidi ya Uturuki ni jambo ambalo halitaepukika.

Hapana shaka kuwa, kutokana na kuweko tofauti kubwa za kiutamaduni baina ya Uturuki na madola ya Ulaya, suala la kujiunga nchi hiyo na Umoja wa Ulaya daima limekuwa likikumbwa na vizingiti. Ukweli wa mambo ni kuwa, Uturuki imejitolea kwa hiari kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya ambao unahesabiwa kuwa kalbu ya Wakristo.

Hii ni katika hali ambayo, Profesa Necmettin Erbakan Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki, katika muongo wa 90 alipendekeza mpango wa kuundwa kundi la D-8 la nchi zinazoendelea za Kiislamu, ambapo kwa kuweko muungano baina yao zinaweza kuwa na mchango na ushawishi mkubwa ulimwenguni. Lau kama viongozi wa Uturuki wangechaguua mkondo wa kulifanya kundi la D-8 kuwa amilifu, kundi hili hii leo lingekuwa hata na kiti maalumu katika Umoja wa Mataifa.

Tags