Mwanahabari wa Marekani ashitakiwa kwa ugaidi Myanmar
Mwandishi wa habari wa Marekani ambaye anazuiliwa na vyombo vya usalama nchini Myanmar kwa miezi kadhaa sasa amefunguliwa mashitaka ya ugaidi na uhaini, na yumkini akahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Danny Fenster, Meneja Mhariri wa gazeti la Frontier Myanmar mwenye umri wa miaka 37, alikamatwa na maafisa usalama mwezi Mei huu akijaribu kutoroka Myanmar.
Than Zaw Aung, wakili wa mwanahabari huyo amesema mteja wake amefunguliwa mashitaka mengine mawili, chini ya Sheria ya Kupambana na Ugaidi ya Myanmar. Sheria hiyo inapiga marufuku kuwasiliana na makundi yaliyoorodheshwa rasmi na serikali ya Myanmar kuwa ya kigaidi.

Mwanahabari huyo wa Marekani tayari alikuwa anaamdamwa na mashitaka mengine kadhaa, kama ya kushajiisha uasi dhidi ya jeshi linalotawala Myanmar kwa sasa, na pia kukiuka Sheria ya Uhamiaji.
Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo. Watu 1,200 wameuawa na maafisa wa usalama wa Myanmar tangu yalipojiri mapinduzi ya kijeshi.