Jeshi la Marekani lilificha mauaji ya watoto na wanawake 64 Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i76890-jeshi_la_marekani_lilificha_mauaji_ya_watoto_na_wanawake_64_syria
Imebainika kuwa, jeshi vamizi la Marekani lilificha kwa makusudi taarifa za kufanyika mashambulizi mawili ya anga yaliyoua makumi ya watoto wadogo na wanawake wa Syria mwaka 2019.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 14, 2021 04:37 UTC
  • Jeshi la Marekani lilificha mauaji ya watoto na wanawake 64 Syria

Imebainika kuwa, jeshi vamizi la Marekani lilificha kwa makusudi taarifa za kufanyika mashambulizi mawili ya anga yaliyoua makumi ya watoto wadogo na wanawake wa Syria mwaka 2019.

Hayo yamefichuliwa na gazeti la Marekani la New York Times katika chapisho lake la jana Jumamosi na kueleza kuwa, mnamo Machi 18 mwaka 2019, wanawake na watoto wasiopungua 64 waliuawa katika hujuma mbili zilizofuatana za jeshi la anga la Marekani karibu na mji wa Baghouz katika mkoa wa mashariki wa Dayr al-Zawr.

Wakili wa jeshi la anga la Marekani ambaye alishuhudia operesheni hiyo amesema anaamini kuwa mashambulizi hayo yana uzito wa kuwa jinai za kivita. 

Kwa mujibu wa New York Times, licha ya wakili huyo kuwasilisha ripoti ya mashambulizi hayo kwa Inspekta Jenerali wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani na Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Baraza la Seneti la nchi hiyo, lakini hakuna uchunguzi wala hatua zozote za maana zilizochukuliwa kufikia sasa.

Hujuma za anga za US dhidi ya Wasyria

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) inayosimamia operesheni za vikosi vamizi vya Marekani katika eneo la Asia Magharibi imehalalisha mauaji hayo ya kinyama ikidai kuwa, hujuma hizo za anga zilifanyika eti kwa lengo la kujihami na eti kwa maslahi ya wapiganaji wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Washington.

Idadi kubwa ya raia wa Syria hususan wanawake na watoto wadodo wameuawa tangu Marekani iivamie nchi hiyo ya Kiarabu mwaka 2014, kwa kisingizio cha kupambana na genge la kigaidi la ISIS (Daesh).