Nov 20, 2021 13:57 UTC
  • Vienna, Austria yageuzwa uwanja wa maandamano ya kupinga karantini na chanjo ya lazima ya corona

Mji mkuu wa Austria, Vienna leo umegeuzwa uwanja wa maandamano ya kupinga uwekaji karantini kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 na upigaji chanjo ya lazima ya ugonjwa huo.

Wiki iliyopita serikali ya Austria ilitangaza karantini ya nchi nzima na kueleza pia kwamba kuanzia Februari mosi 2022, upigaji chanjo ya corona litakuwa jambo la lazima.

Kansela Alexander Schallenberg wa Austria amesema, idadi ya watu waliopigwa chanjo ya Covid-19 nchini humo si ya kiwango cha kutosha na akawatuhumu wale wanaokataa kupigwa chanjo hiyo kuwa wanahujumu mfumo wa afya wa nchi hiyo.

Kansela Alexander Schallenberg

Marufuku ya uendeshaji shughuli mbalimbali itaanza kutekelezwa siku ya Jumatatu ambapo mikahawa, klabu za starehe za usiku na maduka yote yasiyo ya bidhaa za lazima yatafungwa.

Vilevile usomeshaji kupitia madarasani utasimamishwa na shughuli zote za masomo zitarejea tena katika mfumo wa kusomesha kupitia intaneti. Marufuku na karantini hizo zitatekelezwa kwa muda wa wiki tatu lakini zitaangaliwa upya baada ya siku 10.

Kushamiri kwa msambao wa virusi vya corona kumeligeuza bara la Ulaya kuwa kitovu cha maambukizi duniani hususan nchi za Ulaya ya kati ambazo zimelazimika kuweka karantini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza hivi karibuni kuwa  katika kipindi cha wiki iliyopita, idadi ya vifo vilivyosababishwa na maradhi ya Uviko-19 barani Ulaya imeongezeka kwa asilimia tano na kwamba Ulaya ndilo eneo pekee duniani ambalo limeshuhudia ongezeko la vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona.../

Tags