Mazungumzo ya Vienna yakisubiri maamuzi ya maana na ya kimantiki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i77692-mazungumzo_ya_vienna_yakisubiri_maamuzi_ya_maana_na_ya_kimantiki
Mazungumzo yanayohusiana na kuondolewa vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Iran, yalianza Jumatatu ya wiki iliyopita mjini Vienna, Austria. Siku ya Ijumaa mazungumzo hayo yalisimamishwa kwa muda ili kutoa fursa kwa washiriki kurejea katika nchi zao kwa mashauriano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2021 22:54 UTC
  • Mazungumzo ya Vienna yakisubiri maamuzi ya maana na ya kimantiki

Mazungumzo yanayohusiana na kuondolewa vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Iran, yalianza Jumatatu ya wiki iliyopita mjini Vienna, Austria. Siku ya Ijumaa mazungumzo hayo yalisimamishwa kwa muda ili kutoa fursa kwa washiriki kurejea katika nchi zao kwa mashauriano.

Ali Bagheri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kisiasa amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya al Jazeera kwamba, vikwazo vyote vinavyohusiana na mradi wa nyuklia na vikwazo vyote vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran chini ya anwani ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, inabidi viondolewe haraka. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya siasa vile vile amesema, mipango ambayo tumeiwasilisha kwa upande wa pili wa mazungumzo hayo yanaonesha kuwa tuna nia ya kweli ya kutatua tatizo hilo. Mipango hiyo hivi sasa iko kwenye meza ya upande wa pili wa mazungumzo na tunasubiri majibu. Tab'an tunachotarajia ni kuona majibu hayo yanatolewa kwa ushahidi wa kimantiki wa kuonesha nia ya kweli upande huo wa pili kama ilivyoonesha Iran.

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vienna umeandaa mapendekezo mawili katika kalibu ya maudhui mbili zinazohusiana na kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na suala la mradi wa nyuklia na kuyakabidhi kwa kundi la 4+1. Upande huo wa pili wa mazungumzo hayo unapaswa kuchunguza mapendekezo hayo ya Iran na kujiandaa kwa ajili ya mazungumzo mengine yenye nia ya kweli na Jamhuri ya Kiislamu, kuhusu vipengee vilivyomo kwenye mapendekezo hayo.

Ali Bagheri Kani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Ijapokuwa baada ya kupita awamu sita za mazungumzo ya kina na nyeti kuhusu kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, wanadiplomasia na wakuu wa nchi zinashoshiriki kwenye mazungumzo hayo wanaamini kuwa, si jambo lililo mbali kuweza kufikiwa makubaliano ya kurejea pande zote kwenye vipengee vyote vya JCPOA vya mwaka 2015, lakini fursa iliyobakia ya kufikia kwenye mazungumzo yenye mafanikio, si kubwa sana.

Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika mazungumzo ya Vienna amesisitiza kuwa, kuna kanuni katika mazungumzo yoyote yale ambayo inasema, haiwezekani kufikia makubaliano yoyote bila ya kufikiwa kwanza mapatano katika vipengee vyote.

Mtazamo mmoja unasema kuwa, iwapo mapatano ya nyuklia ya JCPOA yatavunjika maana yake itakuwa ni kufeli jitihada za pamoja za mataifa mbalimbali za kulinda ushirikiano wa kimataifa; na kama hilo litatokea, basi madola yote makubwa yanayodai kuwa na nafasi muhimu katika jamii ya kimataifa, yatapata madhara. 

Josep Borrel, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

 

Ni kwa sababu hiyo ndio maana pande ambazo bado zimo ndani ya mapatano ya JCPOA, hazitaki kuona makubaliano hayo yanavunjika. Marekani nayo inasema inataka kurejea kwenye mapatano hayo lakini wakati huo huo haiko tayari kuondoa vikwazo ilivyoiwekea Iran. kinyume kabisa na yanavyosema mapatano ya JCPOA.  Undumilakuwili huo wa Marekani na kupenda kwake kujikumbizia kila kitu upande wake, ndiko kunakokwamisha kufikiwa makubaliano kuhusu mapatano ya JCPOA.

Josep Borrel, mkuu wa siasa za kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema siku ya Jumamosi wakati akiwa mjini Rome Italia kwamba, Umoja wa Ulaya unafanya juhudi za kuhakikisha makubaliano ya JCPOA ambayo mbali na kuwa kwake mapatano ya nyuklia, ni makubaliano pia ya kiuchumi, yanalindwa. Aliongeza kuwa, rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump aliitoa nchi yake kwenye mapatano hayo bila ya kuzingatia matokeo yake mabaya na licha ya kwamba wakati huo Iran ilikuwa imeshikamana kikamilifu na vipengee vya JCPOA.. Mkuu huyo wa siasa za kigeni za Umoja wa Ulaya pia alisema, kama tunataka Iran irejee kikamilifu kwenye mapatano ya JCPOA, inabidi tuipe Tehran kitu ambacho kina daraja sawa na kurejea kwake katika makubaliano hayo.

Ni jambo lililo wazi kuwa, kama kuna nia ya kweli ya kuyafufua kikamilifu makubaliano ya JCPOA, basi hakuna njia nyingine isipokuwa kila upande husika uchukuwe msimamo wa kimantiki na unaokubalika kiakili wa kuyalinda mapatano hayo.