Jimmy Carter: Marekani ni ghala kubwa la ubaguzi wa rangi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i7783-jimmy_carter_marekani_ni_ghala_kubwa_la_ubaguzi_wa_rangi
Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter amesema Donald Trump, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ni mbaguzi wa rangi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 25, 2016 03:02 UTC
  • Jimmy Carter: Marekani ni ghala kubwa la ubaguzi wa rangi

Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter amesema Donald Trump, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ni mbaguzi wa rangi.

Carter ameyaeleza hayo katika mahojiano na gazeti la New York Times na kufafanua kuwa kuna limbiko kubwa la ubaguzi wa rangi lililofichika ndani ya ardhi ya Marekani, na kwamba sehemu moja ya limbiko hilo imedhihrika na kujitokeza hivi sasa, naye Donald Trump anachota fungu lake katika limbiko hilo.

Rais huyo wa zamani wa Marekani amebainisha kuwa kuchaguliwa Barack Obama kuwa Rais wa Marekani ilikuwa ni harakati ya upigaji hatua mbele na kwamba jambo hilo lilikabiliwa na jibu na radiamali za kibaguzi za baadhi ya Warepublican waliopinga na wanaoendelea kupinga mtu mweusi kuwa rais wa nchi hiyo.

Carter ameashiria kashfa za mara kwa mara za miamala miovu na ya kibaguzi ya polisi dhidi ya Wamarekani weusi, idadi kubwa ya wasio na ajira miongoni mwao pamoja na wanaotiwa nguvuni na vyombo vya dola na kufafanua kuwa katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu iliyopita Marekani imebaini kwamba suala la ubaguzi wa rangi halijatatuliwa kwa njia sahihi na kwa kiwango cha kuridhisha nchini humo.

Rais wa zamani wa Marekani ameongeza kuwa Donald Trump, bilionea wa chama cha Republican amepata ardhi yenye rutuba iliyojaa akiba na limbiko la ubaguzi wa rangi; hivyo anachota na kutumia fungu lake.

Aidha amesema kauli ya Trump ya kuwaita Wamexico wahalifu na kwamba anataka kuifunga mipaka ya Marekani ili Waislamu wasiingie nchini humo ni kuzifanyia kejeli na dhihaka haki za msingi za utu.../