Kufichuliwa hitilafu kati ya Berlin na Washington kuhusu Ukraine
Gazeti la Ishpigel la nchini Ujerumani limeripoti kuwa Emily Haber Balozi wa Ujerumani mjini Washington ametuma barua ya siri kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ujerumani akisistiza kuwa Washington inaitambua Ujerumani kama nchi muitifaki asiyeaminika kutokana na kushindwa kutoa ushirikiano unaohitajika kuhusu kadhia ya Ukraine.
Haber pia amebainisha kuwa, si tu katika vyombo vya habari bali ndani ya Kongresi ya Marekani pia wanaamini kuwa serikali ya Ujerumani imeuwa ikiweka vigingi kuhusiana na vikwazo dhidi ya Russia; hasa ikizingatiwa kwamba kitendo cha nchi hiyo cha kuzuia kutumwa silaha Ukraine kutoka Ujerumani kimeibua hasira na ukosoaji katika uwanja huo khususan kutoka kwa wabunge cha chama ca Republican. Emily Haber Balozi wa Ujerumani mjini Washington ameongeza kuwa, msimamo wa Ujerumani unatafsiriwa huko Washington kwamba unatokana na nia ya Berlin kutaka kuendelea kununua gesi ya bei nafuu kutoka Russia.
Bila shaka kufichuliwa barua hiyo ya Balozi wa Ujerumani mjini Washington kumeweka wazi hitilafu kubwa za kimtazamo zilizopo kati ya nchi mbili hizo wanachama wa muungano wa Nato kuhusu namna ya kuamiliana na Russia na vilevile kuiunga mkono Ukraine. Hii ni katika hali ambayo Marekani na muungano wa Nato miezi kadhaa iliyopita zilishadidisha wimbi la kuituhumu Russia kwamba imeazimia kuishambulia Ukraine. Marekani na Nato zinatumia suala hilo kama kisingizio cha kushadidisha pakubwa misaada yao ya kijeshi kwa Kiev; jambo lililobua hitilafu kati ya Berlin na Washington. Marekani si tu imetuma Ukraine mamia ya misaada ya kijeshi, silaha na zana mbalimbali za kivita bali nchi waitifaki wa Washington katika muungano wa Nato kama Uingereza na nchi za pembetatu za Baltic pia zimetuma huko Ukraine maroketi na makombora ya kutungulia vifaru na yale ya angani. Wakati huo huo Berlin huku ikiridhika tu na kutangaza kuunga mkono msimamo wa Nato hivi karibuni ikiwa chini ya mashinikizo ya Washington ilitangaza kuwa itaasisi hospitali ya muda na na kutuma kofia elfu tano aina ya helmet huko Ukraine. Hata hivyo hatua hiyo ya Berlin imekabiliwa na jibu la kejeli kutoka kwa Rais Volodymyr Zelinsky wa Ukraine. Hasa ikizingatiwa kuwa Berlin hadi siku kadhaa zilizopita ilikuwa hairuhusu kuruka katika anga ya Ujerumani ndege zozote zilizobeba silaha kwa ajili ya Ukraine. Wakati huo huo Olaf Scholz Kansela wa Ujerumani aliwahi kusisitiza kuwa msimamo wa nchi hiyo si kutuma silaha hatarishi katika maeneo yanye vita.
Inaonekana kuwa serikali ya shirikisho ya Ujerumani imehitilafiana pakubwa kwa upande wa mitazamo na Marekani na washirika wa Washington ndani ya Nato juuya namna ya kuamiliana na Russia. Japokuwa Berlin imetangaza kuwa haitaruhusu kufanya kazi bomba la gesi la Nord Stream 2 iwapo Russia itaishambulia Ukraine, lakini kwa kuzingatia utegemezi wa asilimia 40 wa nchi za Ulaya kwa gesi ya Russia, viongozi wa Ujerumani wana wasiwasi sana wakihofia kukatwa huduma za usafirishaji gesi ya Russia kama hatua yake ya kulipiza kisasi ikiwa Ulaya itaiwekea Moscow vikwazo vipya.
Katika upande mwingie, kwa kuzingatia msimu wa baridi kali hivi sasa barani Ulaya, kutokea tukio kama hilo kutakuwa na athari mbaya kwa watu wa nchi za Ulaya na kuathiri pia sekta za viwanda na za kudhamini huduma ya umeme. Hii ni kutokana na kuwa uwezo wa kuzalisha nishati ya gesi huko Ulaya hivi sasa umepungua na haukidhi mahitaji ya eneo la Euro na katika Umoja wa Ulaya. Kuhusu wasiwasi huo wa Berlin, baadhi ya nchi washirika wa Ulaya kama Austria pia zimetaka kuondolewa gesi katika vikwazo vipya dhidi ya Russia iwapo nchi hiyo itaishambulia Ukraine.
Alexander Schallenberg Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria anasema: "katika mgogoro wa Ukraine, suala la usafirishaji gesi asilia ya Russia halipasi kujumuishwa katika vikwazo vya Umoja wa Ulaya. Sisi barani Ulaya kwa upande mmoja tunategemea nishati ya Russia; na hatuwezi kubadili hilo mara moja kama tunataka joto na umeme."
Wakati huo huo kitendo cha viongozi wa Ujerumani cha kutangaza misimamo yao kama matamshi ya upendeleo yaliyotolewa na kamanda aliyejizulu wa jeshi la majini la Ujerumani kwa Russia na ya Rais Vladimir Putin wa Russia yamechochea malalamiko ya Washington kuhusu Berlin kuhusiana na suala la Ukraine. Inaonekana kuwa, serikali ya sasa ya Biden pia inatekeleza mwenendo ule ule wa kuibua mivutano kwa visingizio mbalimbali sawa kabisa na wakati wa utawala wa mtangulizi wake huko Marekani yaani Donald Trump ambaye aliibua hitilafu kati ya Washington na Berlin katika nyanja za kisiasa, biashara na kijeshi.