Zelensky adai: Russia itaishambulia Ukraine siku ya Jumatano
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amedai kuwa Russia itatekeleza shambulio dhidi ya Kiev siku ya Jumatano.
Mivutano imeongezeka pakubwa katika eneo katika wiki za karibuni kufuaria baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi kudai kuwa upo uwezekano Russia kutekeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine. Moscow kwa upande wake imetangaza mara kadhaa kwamba haina nia ya kuivamia kijeshi Ukraine bali inachotaka ni kupatiwa dhamana ya kiusalama ambayo itauzuia muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi (Nato) kusonga mbele karibu na mipaka yake.
Shirika la habari la Irna limeripoti kuwa, Rais wa Ukraine ametoa taarifa na kudai kuwa amepokea taarifa kwamba Russia siku ya Jumatano itaishambulia nchi hiyo. Rais wa Ukraine hata hivyo hakutaja chombo cha habari kilichompatia taarifa hiyo na ametangaza kuwa Jumatano ni siku ya umoja na mshikamano. Wakati huo huo televisheni ya CNN imedai kuwa vyombo vya kuaminika vimetangaza kuwa, Russia tayari imetuma baadhi ya makombora yake ya masafa marefu na maroketi katika maeneo itapotekelezea mashambulizi hayo tajwa.