Putin asisitiza, Russia haina nia ya kuingia vitani na Ukraine
-
Rais Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa Rassia aliuambia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Jumanne baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, huko Kremlin kwamba ametoa wito kwa nchi za Magharibi kujiepusha kupeleka silaha za kivita kwenye mipaka ya Russia na kwamba zinapaswa kusitisha upanuzi wa shirika la NATO upande wa Mashariki.
Putin mesisitiza kuwa Russia haitaki vita na kwa sababu hiyo imetoa mapendekezo kadhaa ya kuanza mazungumzo ya kufikia mapatano juu ya usalama jumuishi, japokuwa hadi sasa haijapokea majibu kuhusu mapendekezo hayo.
Wakati huo huo Rais wa Russia ameashiria hali inayotawala mashariki mwa Ukraine na kusema, kinachoendelea huko Donbas ni maangamizi ya kizazi na kwamba serikali ya Kiev inakiuka haki za binadamu kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwabagua watu wanaozungumza lugha ya Kirusi wa Ukraine.
Putin aidha amezungumzia kupitishwa kwa azimio la Duma la kutambua uhuru wa Donetsk na Luhansk na kusema kuwa, bado ana matumaini kuhusu makubaliano ya Minsk na kwamba wakati wa kutekelezwa makubaliano hayo haujapita.
Bunge la Rassia, Duma, siku ya Jumanne lilipitisha azimio hilo kwa kura 351 za ndio, 16 zilipinga na moja haikupiga kura. Azimio hilo limetumwa kwa Rais wa Russia kwa ajili ya kuanza kutekelezwa, na iwapo Putin atalisaini, Russia itatambua rasmi jamhuri za Donetsk na Luhansk.

Sisitizo la Putin kwamba Russia haina nia ya kuingia vitani na Ukraine kwa hakika ni jibu kwa vita vya kisaikolojia na kipropaganda vya nchi za Magharibi hasa Marekani zinazodai kwamba, Moscow imejiweka tayari kikamilifu kuishambulia Ukraine. Marekani kama kinara wa nchi za Magharibi, imekuwa na mchango mkubwa katika vita hivyo vya kipropaganda na hata maafisa wa Washington wamedai kuwa shambulio hilo litafanyika Jumatano, Februari 16.
Hata hivyo, kwa mtazamo wa Moscow, madai haya ni kisingizio tu kinachotumiwa na Marekani na washirika wake wa NATO kuiwezesha zaidi Ukraine kwa silaha na kuzidisha uwepo wa wajeshi ya nchi hizo huko Ulaya Mashariki na katika bahari zinazopakana na Russia, yaani Bahari Nyeusi na Bahari ya Baltic. Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza Jumanne kwamba, mazoezi ya kijeshi ya vikosi vya nchi hiyo huko Belarus yamekamilika, na kwamba mchakato wa kurejea makambini vikosi hivyo umeanza. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema kuwa propaganda za Magharibi kuhusu kuanza vita vya Russia dhidi ya Ukraine zimeshindwa na kufeli. Hata hivyo Washington inaendelea kukariri madai yake yasiyo na msingi. Rais Joe Biden wa Marekani jioni ya Jumanne iliyopita alidai kuwa, uwezekano wa Russia kuishambulia Ukraine bado upo paleple.

Licha ya sera hizo za uchochezi na za kupenda vita za Marekani, nchi kubwa za Ulaya, hasa Ujerumani na Ufaransa, zina wasiwasi kuhusu matokeo mabaya ya vita huko Ulaya Mashariki; kwa sababu hiyo viongozi wa nchi hizo mbili wameweka mbele juhudi za kidiplomasia kwa kufanya safari huko Russia na kukutana na Rais Vladimir Putin. Katika mazungumzo yake na Rais Putin, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alieleza kwamba kuwepo kwa majeshi ya Russia karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ukraine ni tishio na kusisitiza kwamba bado kuna uwezekano wa kufanyika mazungumzo na kukomesha mgogoro wa sasa. Kansela wa Ujerumani amesema kuondoka baadhi ya majeshi ya Russia katika mpaka wa Ukraine ni hatua muhimu. Olaf Scholz amesisitiza kuwa, kwa sasa suala la uanachama wa Ukraine katika shirika la NATO haliko katika ajenda ya shirika hilo.

Kwa utaratibu huo inaonekana wazi kwamba, watu wa Ulaya wanataka kupunguzwa mivutano na kurejeshwa utulivu baina ya Russia na Ukraine na kinyume chake, Marekani inaendelea kupiga ngoma za vita na kuchoea moto huko mashariki mwa Ulaya.