Waliofariki dunia kwa mafuriko nchini Brazil waongezeka hadi 117
(last modified Fri, 18 Feb 2022 11:40:25 GMT )
Feb 18, 2022 11:40 UTC
  • Waliofariki dunia kwa mafuriko nchini Brazil waongezeka hadi 117

Zaidi ya watu 117 wamefariki dunia baada ya siku kadhaa za mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yaliyoharibu barabara na nyumba nchini Brazil.

Gavana Claudio Castro wa Rio de Janeiro, jimbo lililoathirika zaidi na majanga hayo ya kimaumbile yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo amesema, barabara na mitaa ya mji wa Petropolis inashabihiana na 'eneo la vita' na kwamba jimbo hilo halijawahi kushuhudia mvua kubwa za namna hii tokea mwaka 1932.

Gavana Castro amesema jimbo hilo kwa sasa limewekwa katika hali ya tahadhari kwa mvua zingine zinazotazamiwa kunyesha, huku serikali yake ikitangaza siku tatu za kuomboleza vifo hivyo.

Mamlaka za nchi hiyo ya Amerika ya Latini zimetangaza kuwa, watu wengine wengi bado hawajulikani waliko kufuatia mafuriko na maporomoko hayo.

Athari za mafuriko

Taarifa ya mamlaka hizo imeeleza kuwa, watu zaidi ya 850 wamelazimika kuhamishiwa katika makazi ya muda hususan katika maeneo ya shule za umma, baada ya nyumba zao kufukiwa kwenye maporomoko ya udongo au kusombwa na maji ya mafuriko.

Rais Jair Bolsonaro wa Brazil ambaye anatazamiwa leo Ijumaa kumaliza ziara ya siku tatu ya kuzitembelea Russia na Hungary, atautembelea mji wa Petropolis ulioathiriwa na maporomoko ya ardhi na mafuriko hayo kutathmini ukubwa wa majanga hayo.