Zakharova: Oparesheni za Kijeshi za Russia nchini Ukraine si uvamizi
Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, muungano wa kijeshi wa NATO haupaswi kuzitaja oparesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine kuwa ni uvamizi.
Akizungumza Jumamosi usiku, Zakharova amesema: "Kwa kuzingatia kushindwa nchi za NATO kufanya mazungumzo na kutokuwa na irada ya kuimarisha usalama wa Ulaya kwa msingi wa mlingano katika usalama, sasa zinajaribu kutoa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti Russia imeivamia Ukriane."
Zakharova amesema kabla ya nchi za NATO kutaka Russia itoe majibu kutokana na oparesheni zake nchini Ukraine zenye lengo la kuondoa muundo wa kijeshi Ukraine, inapaswa kufafanua kuhusu chokochoko zake za kijeshi. Aidha amesema NATO inapaswa kutoa jibu ni kwa nini imekataa kuushawishi utawala wa Ukraine ufuatilie njia za amani katika kutatua matatizo yaliyojitokeza.
Nchi kadhaa za Magharibi zikiwemo Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya, zimetangaza vikwazo vikali dhidi ya Russia kufuatia oparesheni za kijeshi za nchi hiyo huko Ukraine. Rais Joe Biden wa Marekani ametetea vikwazo hivyo na kudai kuwa kama silaha ya vikwazo haitumiki basi kutaibuka vita vikuu vya tatu vya dunia. Amevitaja vikwazo hivyo vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Russia kuwa vikali zaidi katika historia.
Katika sehemu ya vikwazo hivyo, imetangazwa kuwa benki kadhaa za Russia zitaondolewa kwenye mfumo wa malipo wa kimataifa wa SWIFT. Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema hatua hiyo itahakikisha kwamba benki zitasitisha uhusiano wao na mfumo wa kimataifa wa kifedha na Russia ili kutatiza uwezo wake wa kufanya kazi kimataifa.
Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo Jumapili kwa mara ya nne ndani ya wiki moja kujadili kadhia ya Ukriane.
Oparesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine zilianza Alkhamisi iliyopita baada ya Rais Vladimir Putin wa Russia kutangaza kwamba jeshi la nchi hiyo limeanzisha "operesheni maalumu ya kijeshi" katika eneo la Donbass. Alisema lengo la operesheni hiyo ni kuiondoa Ukraine katika hali ya kijeshi na kwamba hana nia ya kuvamia ardhi ya nchi hiyo.