Ombi la Ukraine la kujiunga na Umoja wa Ulaya limekubaliwa
(last modified Wed, 02 Mar 2022 13:42:11 GMT )
Mar 02, 2022 13:42 UTC
  • Ombi la Ukraine la kujiunga na Umoja wa Ulaya limekubaliwa

Bunge la Ulaya limepitisha ombi la Ukraine la kujiunga na jumuiya hiyo kwa kura 637 za 'ndiyo' 13 za 'hapana' huku wajumbe 26 wakiamua kutopiga kura.

Siku ya Jumanne, nchi nane wanachama wa EU zilitaka yafanyike majadiliano ya haraka kuhusu uwanachama wa Ukraine katika umoja huo.

Jumapili iliyopita, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliuomba Umoja wa Ulaya uafiki ombi la nchi yake la kupatiwa uwanachama wa haraka kwa kutumika utaratibu maalumu.

Hata hivyo kukubaliwa ombi la Ukraine na bunge la Ulaya hakumaanishi Kiev kuwa mwanachama rasmi katika jumuiya hiyo, bali kwa kupigiwa kura na kupitishwa ombi hilo, sasa mchakato wa nchi hiyo kujiunga na EU utakuwa umeanza.

Kwa utaratibu wa kawaida, nchi inayoomba uwanachama wa kujiunga na Umoja wa Mataifa inatakiwa itimize masharti mbalimbali yanayokidhi vigezo vya Copenhagen, ikiwemo kuwa na soko la uchumi huru, demokrasia thabiti na utawala wa sheria pamoja na kukubali kanuni na sheria zote za Umoja wa Ulaya ikiwemo ya sarafu ya yuro.

Baada ya viongozi wa eneo la Donbas nchini Ukraine kuiomba Russia iwatumie misaada ya kijeshi kulingana na mikataba ya ushirikiano iliyoko baina yao, siku ya Alkhamisi ya tarehe 24 Februari, Rais Vladimir Putin wa Russia alitangaza katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni  ya nchi hiyo kuanza kwa operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbas.

Hivi sasa Russia inaendelea kuandamwa na vikwazo vikali vya Marekani na waitifaki wake kwa sababu ya kuwaunga mkono Waukraine wenye asili ya Russia wa mashariki ya Ukraine na kuunga mkono uamuzi wa maeneo ya Donetsk na Luhansk kutangaza kujitenga na Ukraine.../

Tags