Spika wa Bunge la Russia: Rais wa Ukraine amekimbilia Poland
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81036-spika_wa_bunge_la_russia_rais_wa_ukraine_amekimbilia_poland
Spika wa Bunge la Russia maarufu kwa jina la Duma amesema kuwa, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amekimbilia nchi jirani ya Poland.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2022 04:02 UTC
  • Spika wa Bunge la Russia: Rais wa Ukraine amekimbilia Poland

Spika wa Bunge la Russia maarufu kwa jina la Duma amesema kuwa, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amekimbilia nchi jirani ya Poland.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Vyacheslav Volodin, Spika wa Bunge la Russia akisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa za uhakika alizo nazo, rais wa Ukraine amekimbilia Poland.

Mwanzoni mwa vita vya Russia dhidi ya Ukraine, spika huyo wa Bunge la Russia alisema kuwa, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amekimbia mji mkuu Kyiv na kujificha katika mji wa Lviv wa kusini magharibi mwa Ukraine. Kwa mujibu wa Spika wa Bunge la Russia, video zote zinazomuonesha Zelenskyy akiwa Kyiv, zimerekodiwa zamani kabla hajakimbia.

Athari za vita nchini Ukraine

 

Huko nyuma nchi kadhaa za Magharibi zikiwemo Marekani na Uingereza zilidai kuwa ziko tayari kumpokea Zelenskyy kama mkimbizi wa kisiasa na kumruhusu kuunda serikali yake nje ya Ukraine. Gazeti la Times la mjini London Uingereza jana Ijumaa lilidai pia kwamba, hadi hivi sasa yameshafanyika majaribio yasiyopungua matatu ya kumuua Zelenskyy lakini yameshindwa.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, serikali ya Ukraine inaendelea kuwapa hifadhi magaidi wa kimataifa, wakiwemo wale waliotenda jinai kubwa dhidi ya raia wa Syria.

Siku chache zilizopita, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alizishukuru nchi waitifaki kwa kuendelea kutuma silaha na zana za vita nchini humo na kusema kundi la kwanza la wapiganaji elfu 16 wa kigeni limeshawasili nchini Ukraine.

Ripoti zinasema kuwa, operesheni maalumu ya jeshi la Russia nchini Ukraine ambayo inafanyika kwa ajili ya kuipokonya silaha serikali ya nchi hiyo, inalenga pia kupambana na magenge ya kigaidi.