Mkurugenzi Mkuu wa WHO: Migogoro yote duniani inapasa ipewe umuhimu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema, wakati macho yote yameelekezwa kwenye mgogoro wa Ukraine, zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini Afghanistan wanahitaji msaada.
Mgogoro wa Ukraine ulianza Februari 24, huku Russia, ambayo imeivamia kijeshi nchi hiyo ikisisitiza kuwa sababu ya kuchukua hatua hiyo ni kuipokonya silaha Ukraine na kuepusha kuanza vita vya dunia.
Dkt. Tedros Adhanom, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema, suluhu na amani ndio njia pekee ya kutatua migogoro yote iliyopo hivi sasa duniani.
Adhanom ametoa sisitizo hilo alipohutubia Alkhamisi kwa njia ya video kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani amelitaka Baraza la Usalama lichukue hatua kwa ajili ya kusitishwa vita na kutafutwa njia ya ufumbuzi wa kisiasa katika kadhia ya Ukraine na akaongeza kwamba, kuchukua muda mrefu zaidi vita hivyo hakuunufaishi upande wowote bali dunia itaendelea kushuhudia mateso kwa watu wanaoathirika zaidi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo Dkt. Tedros Adhanom amesema, kama alivyoeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ni asilimia 36 tu ya fedha za msaada zinazohitajika zimekusanywa huku watu wa Afghanistan wakikabiliwa na hali mbaya ya utapiamlo, mbali na matatizo mengine yaliyoikumba nchi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO amekumbusha pia kuhusu mgogoro wa Ethiopia, ambako watu milioni sita katika eneo la Tigray wamewekewa mzingiro, licha ya kupita siku 500 za mgogoro wa janga la uhaba wa chakula na huduma za afya linalowakabili watu hao.
Halikadhalika ameashiria hali ya Syria ambako watu zaidi ya milioni 12 wanahitaji msaada wa huduma za afya, wakati nusu ya wahitaji hao ni watoto wadogo.
Aidha, Dkt. Adhanom amezungumzia maafa ya Yemen ambako takriban theluthi mbili ya watu wa nchi hiyo na ambao ni zaidi ya watu milioni 20 nao pia wakiwa wanahitaji msaada wa huduma za afya; na akasisitiza tena kwamba suluhu na amani ndio njia pekee ya ufumbuzi wa migogoro yote hiyo.../