Papa Francis atoa wito wa kukomesha vita nchini Ukraine
-
Papa Francis
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani ametoa wito wa kusitishwa vita nchini Ukraine.
Papa Francis ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia juhudi za kuhitimishwa vita nchini Ukraine akisema hakuna kitu kinachohalalisha kuendelezwa vita hivyo.
Papa Francis pia ametaja ghasia dhidi ya Waukraine kuwa za kinyama na za kudhalilisha, akisema kuwa mzozo wa wakimbizi nchini Ukraine unazidi kuwa mbaya siku hadi siku.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema katika ripoti yake ya jana Jumapili kwamba, hadi hivi sasa Waukraini milioni tatu na laki tatu na 28,692 wameikimbia nchi hiyo tangu Februari 24 mwaka huu wakati Russia ilipoanzisha vita dhidi ya nchi hiyo ya Ulaya. Asilimia 90 ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto.
Tarehe 24 mwezi uliopita wa Februari Russia ilianzisha operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine baada ya eneo la Donbass mashariki mwa Ukraine kuiomba Russia msaada wa kijeshi kwa mujibu wa makubaliano ya ushirikiano kati yao.
Russia imetangaza kuwa haina nia ya kuikalia kijeshi Ukraine na kwamba inakusudia kuipokonya silaha, kuiondoa katika mikono ya mafashisti na kizuia vita ya kimataifa. Vilevile Moscow inapinga sera za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO za kujipanua upande wa Mashariki hadi kwenye mipaka ya Russia.