Guterres: Dunia inasuasua kuhusu janga la hali ya hewa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, jana alisema kuwa, ulimwengu unajikongoja kuhusu janga la hali ya hewa huku nchi zilizostawi kiuchumi duniani zikiruhusu kuongezeka uchafuzi wa mazingira kupitia gesi ya carbon katika hali ambayo uchafuzi wa mazingira unapasa kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameuambia Mkutano wa Uendelevu huko London kwamba, lengo la kuokoa sayari ya dunia kwa kupunguza ongezeko la joto duniani kwa nyuzi joto 1.5 (34.7 Fahrenheit) linasuasua. Tume ya IPCC ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi imeeleza kuwa, ili kuweza kutimizwa lengo hilo, hewa chafu ya carbon inapasa kupunguzwa kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030.
Antonio Guterres ameongeza kuwa, hata kama mataifa mbalimbali yataheshimu ahadi mpya zilizofanyiwa marekebisho chini ya Mkataba wa Paris, uzalishaji wa gesi chafu bado unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 14 kabla ya muongo huu kuisha.
Wakati huo huo, wanasayansi wanasema janga hilo linaweza kuepukika iwapo dunia itachukua hatua za haraka.
Kuna matumaini kwamba kupunguzwa kwa kiwango kikubwa zaidi cha hewa chafu kunaweza kusaidia kuzuia ongezeko la viwango vya joto duniani.
Akiunga mkono matokeo ya utafiti ya wanasayansi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema: "iwapo tutaweka pamoja nguvu tunaweza kuepuka janga la ongezeko la joto katika sayari ya dunia.