Apr 07, 2022 07:37 UTC
  • Biden kwa mara nyingine tena ametaka kufukuzwa Russia katika G-20

Janet Yellen Waziri wa Fedha wa Marekani ameeleza kuwa, iwapo Russia itashiriki katika mikutano ya kundi la G-20 Marekani haitahudhuria mikutano hiyo. Amesema: Rais Joe Biden anataka Russia ifukuzwe ndani ya G-20.

Akihutubia jana usiku mbele ya Kamati ya Huduma za Fedha ya Bunge la Wawakilishi la Marekani, Yellen amesema kwamba amewaeleza wazi Mawaziri wengine wa Fedha wa nchi wanachama wa kundi la 20 kuhusu misimamo ya Marekani.

Waziri wa Fedha wa Marekani 

Rais wa Marekani mwezi uliopita pia alisema katika mkutano na waandishi wa habari huko Brussels kwamba: Russia ni lazima ifukuzwe katika kundi la G-20 lakini akaongeza kuwa hata hivyo nchi wanachama zinapasa kuafikiana kwanza kuhusu suala hilo. 

Kikao kijacho cha wakuu wa G-20 kimepangwa kufanyika mwezi Novemba huko Indonesia. Kabla ya kufanyika kikao hicho tajwa, mawaziri wa kundi hilo watatafanya vikao kadhaa. Kundi la G-20 au kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa duniani ni kundi linaloundwa na Mawaziri wa Uchumi na Fedha na Magavana wa Benki Kuu za nchi 20 zenye uchumi mkubwa duniani.

Kundi hilo linaundwa na madola yenge nguvu duniani katika uga wa kiuchumi; ambapo nchi hizo kwa pamoja zinachangia asilimia 85 ya uchumi wote wa dunia na huku zikiwa na theluthi mbili ya idadi ya watu duniani.

Tags