Watoto 400 wajeruhiwa hadi hivi sasa tangu kuanza vita vya Ukraine
Shirika lisilo la kiserikali la Save The Children limetangaza kuwa, karibu watoto 400 wameuawa na kujeruhiwa katika wiki saba za vita vya Ukraine.
Shirika la habari la IRNA limetangaza habari hiyo leo na kulinukuu shirika la Save The Children likisema kuwa, karibu thuluthi mbili ya watoto milioni 7.5 wa Ukraine wamekuwa wakimbizi. Kati ya hao, milioni 2.8 wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi na milioni 2 wengine wamekimbilia nje ya nchi.
Hayo yameripotiwa katika hali ambayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, hivi sasa wanadiplomasia wa Ukraine nje ya nchi hiyo wanaendesha kampeni kubwa ya kutumia mamluki na magaidi wa kigeni katika vita dhidi ya wanajeshi wa Russia.
Shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kumnukuu naibu waziri huyo wa mambo ya nje wa Russia akisema leo mbele ya waandishi wa habari kuwa, hali ya wananchi wa Ukraine itazidi kuwa mbaya kutokana na mamluki na magaidi kutoka nchi za Ulaya na Asia Magharibi kumiminwa nchini humo.
Vile vile na katika uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amesema kuwa, London imeamua kutoa mafunzo ya kijeshi kwa vikosi vinavyoshiriki kwenye mapigano dhidi ya Russia huko Ukraine.
James Heeley ameiambia Radio LBC kwamba, Uingereza imetenga magari 120 ya deraya kwa ajili ya kuwapa mafunzo askari wanaopigana vita dhidi ya Russia nchini Ukraine na imetenga fedha nyingi za kuisaidia kijeshi Ukraine yakiwemo pia makombora ya kutungulia ndege na vifaru pamoja na ndege kadhaa zisizo na rubani aina ya NLAW.
Aidha London imesema itaipa Ukraine makombora mengine 800 ya kupigia vifaru.