Apr 16, 2022 02:39 UTC
  • Mhalifu mwenye misimamo mikali achoma moto Qurani Tukufu Sweden

Mhalifu mmoja mwenye misimamo ya kufurutu ada wa mrengo wa kulia nchini Sweden amechoma nakala inayoaminiwa ni ya Qurani Tukufu katika mtaa ambao akthari ya wakazi wake ni Waislamu.

Rasmus Paludan, kinara wa chama cha Stram Kurs alikuwa ameandamana na askari polisi wa Sweden ambao hawakuonekana kuchukua hatua yoyote ya kumzuia mhalifu huyo asiivunjie heshima Qurani Tukufu, bali hata walionekana wakimpa ulinzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, tukio hilo lilifanyika juzi Alkhamisi katika mji wa Linkoping ulioko kusini mwa Sweden, ambapo Paludan alipuuza makelele na malalamiko ya wapita njia na mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika alikokuwa, wakimuasa asifanye kitendo hicho cha kishenzi na kichochezi.

Mikail Yuksel, mwanasiasa aliyeasisi Chama cha Rangi Tofauti (Party of Different Colors) nchini Sweden, ambaye ni mzawa wa Uturuki amesema inasikitisha vitendo vya aina hii vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vinavyofanywa na wanasiasa wenye misimamo mikali tena chini ya ulinzi wa polisi vimekithiri nchini humohususan katika maeneo ya Waislamu.

Katika miezi ya karibuni Sweden imeshuhudia matukio kadhaa ya hujuma na mashambulio dhidi ya Waislamu, maeneo yao matakatifu na kuvunjiwa heshima pia kitabu kitukufu cha Qurani.

Msikiti Sweden; Idadi ya Waislamu inaongezeka nchini humo licha ya Islamophobia

Oktoba mwaka 2020, vijana kadhaa wa Sweden wenye misimamo ya kufurutu mpaka walifanya kitendo cha kishenzi cha kuivunjia heshima Qurani Tukufu kwa kuchukua msahafu na kuuchoma moto mbele ya jengo la bunge la nchi hiyo.

Aidha Agosti mwaka huohuo, Msahafu mwengine ulichomwa moto katika maandamano haramu na yasiyo na kibali yaliyofanywa na makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu mpaka katika mji wa Malmo nchini Sweden.

Tags