Mwanandondi Muhammad Ali aaga dunia akiwa na miaka 74
Bingwa wa ndondi raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Muhammad Ali ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 74.
Bob Gunnell, msemaji wa familia ya marehemu Muhammad Ali amesema nyota huyo wa masumbwi ameaga dunia katika hospitali moja mjini Phoenix jimbo la Arizona, alikolazwa tangu Alkhamisi iliyopita kutokana na matatizo ya kupumua. Imearifiwa kuwa, matatizo hayo ya kupumua yalitokana na ugonjwa wa kutetemeka alioupata tangu mwaka 1984. Msemaji wa familia ya Muhammad Ali amewashukuru wote waliosimama na nyota huyo wa ndondi alipokuwa anaugua hadi wakati wa kifo chake na kusisitiza kuwa kwa sasa familia hiyo inahitaji faragha. Taarifa ya familia ya mwanamasumbwi huyo imesema bingwa huyo mara 3 wa mashindano ya kimataifa ya Olimpiki atazikwa nyumbani kwake mjini Louisville, eneo la Kentucky.
Itakumbukwa kuwa, bingwa huyo wa ndondi aliyejiunga na mchezo huo akiwa na umri wa miaka 12, alifahamika kama Cassius Clay, lakini akabadilisha jina na kuitwa Muhammad Ali baada ya kujiunga na dini tukufu ya Kiislamu mwaka 1964.