Russia: Israel iache mashambulizi dhidi ya Syria au isubiri matokeo mabaya
Balozi wa Russia nchini Syria amelaani vikali jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kufanya shambulio katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus, mji mkuu wa Syria.
Alexander Efimov ametoa indhari hiyo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na gazeti la al-Watan linalochapishwa kwa lugha ya Kiarabu na kueleza kuwa: Israel inapaswa kukomesha mashambulizi dhidi ya Syria au isubiri matokeo mabaya ya jinai zake.
Amesema Tel Aviv inapaswa kusitisha mara moja vitendo vyake hivyo viovu vinavyohatarisha usalama wa ndege za abiria na sekta ya uchukuzi wa anga kwa ujumla.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amekosoa operesheni ya kijeshi ya Uturuki ndani ya ardhi ya Syria na kusisitiza kuwa, harakati za kijeshi za Akara zinakiuka mamlaka ya kujitawala Damascus, na pia zinakanyaga wazi sheria za kimataifa.
Hivi karibuni, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova alisema kuwa, kwa mara nyingine tunalazimika kusema kuwa, kuendelea kushambuliwa ardhi ya Syria ni kinyume na sheria zote za kimataifa na ni jambo lisilokubalika kabisa.
Ijumaa usiku, jeshi la Israel lishambulia kwa makombora kadhaa baadhi ya maeneo ya kusini mwa Damascus hususan uwanja wa ndege wa mjini huo, kutokea kwenye milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.