UN: Kufukuzwa Wapalestina eneo la Masafer Yatta ni jinai ya kivita
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa kufukuzwa kwa Wapalestina kutoka eneo la Masafer Yatta, kusini mwa Ukingo wa Magharibi, kunaweza kuwa sawa na kuwalazimika kuyahama makazi yao, jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Nne wa Geneva na hivyo kuzingatiwa kuwa ni uhalifu wa kivita.
Takriban Wapalestina 1,150 katika eneo la Masafer Yatta kwenye Ukingo wa Magharibi wapo hatarini kufukuzwa ili jeshi la Israel liweze kujitengenezea eneo lake la mafunzo ya ufyatuaji risasi.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ilionya jana Alhamisi kwamba sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu zinakataza kuwahamisha kwa lazima raia kutoka au ndani ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kwamba mamlaka ya Israel lazima isitishe hatua zote za kutumia mabavu, ikiwa ni pamoja na kuhamisha raia kwa mabavu na uharibifu unaofanyika kwa mpangilio maalumu.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu pia imesema familia 215 za Wapalestina zenye watu 1,150 wakiwemo watoto 569 hivi sasa zinaishi katika eneo la Masafer Yatta na zinakabiliwa na tishio la kubomolewa nyumba zao pamoja na vurugu za walowezi ambao wanaishi katika miji iliyo karibu na eneo hilo.
Taarifa ya OCHA imesema: Walowezi hao wa Kiyahudi wanafunga barabara katika eneo hilo, kuwashambulia wachungaji na kuchoma moto mazizi na malisho yao.
Tangu muongo wa themanini, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilitangaza eneo lilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu la Palestina la Masafer Yatta kuwa ni "Medani ya Ufyatuaji Risasi 918" ili kupanua eneo lake la mafunzo ya kijeshi.
Kufukuzwa kwa wakazi wa eneo hili, ikiwa kutatekelezwa, kutakuwa uhamiaji mkubwa zaidi wa kulazimishwa wa Wapalestina tangu 1967, lakini hadi sasa wakazi wa asili wa eneo hilo wamekataa kutoka kwenye makazi yao kwa matumaini kwamba jamii ya kimataifa itaingilia kati la kusitisha jinai za utawala haramu wa Israel.