Jaribio la Biden kuhalalisha safari yake ya Saudi Arabia
(last modified Tue, 12 Jul 2022 01:25:34 GMT )
Jul 12, 2022 01:25 UTC
  • Jaribio la Biden kuhalalisha safari yake ya Saudi Arabia

Rais Joe Biden wa Marekani amedai katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la Washington Post kwamba katika kipindi cha miezi 18 ya uongozi wake, eneo la Asia Magharibi limekuwa shwari na salama zaidi kuliko hapo awali. Biden ameyasema hayo katika jitihada zake za kujaribu kuhalalisha safari yake tarajiwa nchini Saud Arabia.

Katika safari hiyo Biden anatarajiwa kutembelea Saudi Arabia na kukutana na viongozi wa nchi hiyo; jambo ambalo limekosolewa sana ndani na nje ya Marekani kwenyewe. 

Uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia umedorora katika miaka michache iliyopita kutokana na sababu mbalimbali, kama vile rekodi mbaya za haki za binadamu ya Riyadh, mauaji ya mwandishi wa habari wa Washington Post, Jamal Khashoggi na matamshi ya huko nyuma ya Biden aliyesisitiza udharura wa kutengwa utawala wa Saudi Arabia kutokana an rekodi yake ya kutisha ya ukiukaji wa haki za binadamu hususan mauaji ya mwandishi habari, Jamal Khashoggi.

Itakumbukwa kuwa, wakati anagombea urais, Joe Biden aliwaambia Wamarekani kuwa mauaji ya mwandishi huyo wa habari katika ubalozi wa Saudia nchini Uturuki yanaleta udharura wa kutengwa utawala wa Riyadh katika medani ya kimataifa. Biden aliahidi kuwa atahakikisha kuwa suala hilo linafanyika. Vilevile aliilaumu Saudi Arabia kwa kukosa utu na kuwa kinara wa kuvunja haki za binadamu.

Baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa Marekai pia Biden alichapicha ripoti ya mashirikia ya ujasusi ya nchi hiyo ambayo yalimtambulisha mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman kuwa ndiye aliyepanga na kuamuru mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi. 

Wakosoaji wa safari ya Biden huko Saudi Arabia wanasema, kilicho muhimu kwa rais huyo wa Marekani ni mafuta na haja ya Washington kwa Saudi Arabia. Kinyume na madai yote ya hapo awali ambapo alimtangaza Bin Salman kuwa ni muuaji na Saudia kuwa ni kinara wa uvunjaji wa haki za binadamu, Biden ameamua kuitembelea nchi hiyo na atajadili masuala kama vile mafuta, mgogoro wa Yemen, kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na uhusiano kati ya Israel na Saudi Arabia.

Wakiikosoa safari hiyo, wajumbe wa Baraza la Seneti la Marekani wameandika katika barua iliyotumwa kwa rais wa nchi hiyo wakisema kwamba: "Hatuwezi kumruhusu Muhammed bin Salman kufikiria kwamba anaweza kutawala bila kuadhibiwa." 

Ni kwa kuzingatia shutuma nyingi zilizotolewa kuhusu safari ya sasa ya Biden huko Saudia, ndipo kiongozi huyo akajaribu kutetea ziara hiyo katika mahojiano na makala yake kwenye gazeti la Washington Post. Katika mkondo huo Biden amedai kuwa wakati wa uongozi wake, eneo la Asia Magharibi limekuwa salama na kuungana zaidi, madai ambayo yamekosolewa hata na maafisa wa zamani wa Ikulu ya White House kama Mike Pompeo, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Donald Trump.

Tunaweza kusema kuwa, safari ya Biden eneo la Asia Magharibi itafanyika huku sera za vikwazo za Marekani na mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran zikiwa zimeshindwa, na jeshi la Marekani limeondoa kwa fedheha au kwa maneno mengine, limekimbia Afghanistan. Sera za Marekani zimefeli na kushindwa pia katika nchi za Iraq na Syria, na vita vya Yemen bado vinaendelea. Pamoja na haya yote Biden anadai kuwa Marekani imekuwa sababu ya kurejeshwa usalama na utulivu katika eneo Magharibi mwa Asia!

Mbali na kufeli sera za Marekani katika Mashariki ya Kati, kwa sasa, vita kati ya Russia na Ukraine na uhaba wa mafuta na nishati pia vimeathiri dunia nzima. Ikumbukwe kuwa, miongoni mwa sababu muhimu za safari ya Biden nchini Saudi Arabia ni kujaribu kuishawiashi nchi hiyo na washirika wake wasambaza mafuta zaidi katika masoko ya bidhaa hiyo. 

Joe Biden

Ingawa maafisa wa serikali ya Marekani na vyombo vya habari vimekuwa vikijaribu kuhalalisha safari ya Biden katika eneo la Asia Magharibi, lakini ukweli ni kwamba, hali ya nchi za eneo hilo inaashiria kushindwa kwa sera za Ikulu ya White House. Jambo lisilo na shaka ni kwamba, sera za Marekani eneo la Asia Magharibi hazijawahi kuwa za kujenga usalama, na daima zimekuwa zikisababisha ukosefu wa amani kwa mataifa ya eneo hilo.

Tags