Kusimamishwa usafirishaji wa gesi ya Russia kwenda Ulaya
(last modified Thu, 14 Jul 2022 03:18:39 GMT )
Jul 14, 2022 03:18 UTC
  • Kusimamishwa usafirishaji wa gesi ya Russia kwenda Ulaya

Usafirishaji wa gesi ya Russia kwenda Ujerumani kupitia bomba la "Nord Stream 1" katika Bahari ya Baltic, ulisimamishwa Jumatatu kwa muda wa siku 10.

Kampuni ya Russia Gazprom, ambayo hivi karibuni ilitangaza kuwa kutokana na kuchelewa kwa ukarabati uliokuwa utekelezwe na makampuni ya Ujerumani na Kanada, imepunguza kwa kiasi kikubwa usambazaji wa gesi kupitia bomba la Nord Stream 1. Imesema imesitisha kabisa kusafirisha gesi ya Russia kwenda Ulaya  kwa ajili ya ukarabati wa mitambo na mifumo ya otomatiki. Hayo yanajiri wakati ambapo Moscow ilikuwa imeonya mara kwa mara kwamba ucheleweshaji na kutoshirikiana kwa nchi za Magharibi kunaweza kusababisha kusimamishwa kabisa mtiririko wa gesi kupitia bomba hilo.

"Nord Stream 1" kila mwaka husafirisha takribani mita za ujazo bilioni 55 za gesi hadi kaskazini mwa Ujerumani na kutoka huko hadi nchi mbalimbali za Ulaya, ambayo ni zaidi ya asilimia 40 ya mahitaji ya gesi ya bara la Ulaya.

Kufuatia uamuzi wa hivi karibuni wa kampuni ya Russia ya Gazprom, nchi za Umoja wa Ulaya na hasa Ujerumani zimeingia katika mgogoro mkubwa wa nishati. Nchi hizo zina wasiwasi kuhusu msimu wa baridi kali mwaka huu ambao unaweza kuandamana na mgogoro mkubwa wa kijamii na kiuchumi kutokana na ukosefu au uhaba wa gesi huko Ulaya. Kukatwa kwa gesi hiyo kumesababisha nchi za Ulaya kutumia kiasi cha akiba ya gesi ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya msimu wa baridi kali. Hata baadhi ya nchi za Ulaya zinafikiria kurejea uzalishaji wa makaa ya mawe au kutumia vyanzo mbadala. Kwa mfano Ujerumani imetangaza kuwa itaunganisha mitambo yake ya nishati ya makaa ya mawe kwenye gridi ya taifa ili kuokoa matumizi ya gesi.

Baada ya kuanza vita vya Ukraine na Russia, nchi za Ulaya zilifuata kibubusa amri ya  Marekani na kuiunga mkono Ukraine sambamba na kuiwekea Russia vikwazo vizito.

Njia ya bomba la gesi la Nord Stream

Pamoja na mambo mengine, nchi hizo zilizungumzia suala la kupunguza ununuzi wa mafuta ya petroli na gesi kutoka Russia ili kuishinikiza Moscow kifedha kwa matumaini kuwa ingesitisha oparesheni zake za kijeshi huko Ukraine. Lakini vikwazo hivyo hadi sasa vimetoa matokeo kinyume na ilivyotarajiwa, na sasa hali ni ngumu katika nchi za Ulaya ambazo zinategemea sana vyanzo vya nishati vya Russia.

Katika miezi ya hivi karibuni, Ulaya imekabiliwa na ongezeko kubwa la bei ya gesi kutokana na mzozo wa mafuta uliosababishwa na vikwazo dhidi ya Russia. Kwa mujibu wa maafisa wa Ujerumani, vituo vya kuhifadhi gesi nchini humo kwa sasa vimefika kiwango cha asilimia 61 ambayo ni chini kuliko kawaida kwa msimu huu, na ikiwa mauzo ya gesi ya Russia yatasitishwa, Ujerumani itakuwa na gesi ya kutosha kwa miezi miwili tu.

Bertram Brossardt, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Viwanda cha Jimbo la Ujerumani la Bavaria, amezungumzia kadhia hiyo na kusema: "Ukosefu wa ghafla wa uagizaji wa gesi kutoka Russia unaweza kusababisha kutoweka nafasi za ajira zipatazo  milioni 5.6 katika nchi hii."

Kwa hakika, mgogoro wa gesi utakuwa na matokeo mabaya sana kwa nchi za Ulaya. Ongezeko la bei ya mafuta, ongezeko la gharama za uzalishaji, kupungua kwa ukuaji wa uchumi na matokeo yake, kudhoofika kwa nafasi ya kiuchumi ya Ulaya katika uchumi wa dunia, pamoja na ongezeko la mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira, ni miongoni mwa madhara makubwa ya kiuchumi yanayotakana na kukatishwa mtiririko wa gesi ya Russia kwenda Ulaya.

Kituo cha Uingereza cha Utafiti wa Uchumi na Biashara (CEBR) kimechapisha ripoti kuhusu hali mbaya ya kiuchumi itakayolikumba bara Ulaya na kusema: Mdororo mkubwa wa kiuchumi kutokana na kukatika kwa gesi ya Russia ni hatari isiyoepukika. Sambamba na kusimamishwa kwa mauzo ya nje ya gesi ya Russia kwenda Ulaya kuna hatari ya kudhoofika uchumi wa Ulaya katika msimu ujao wa baridi kali.

Viktor Orban, Waziri Mkuu wa Hungary

Viktor Orban, Waziri Mkuu wa Hungary, hapo awali alionya kwamba Ulaya inakaribia kutumbukia katika mgogoro wa kiuchumi duniani kutokana na vikwazo dhidi ya Russia. Amesisitiza kuwa kupiga marufuku uagizaji wa gesi kutoka Russia kunaweza kuangamiza uchumi wa Ulaya.

Sasa Ulaya inakabiliwa na mgogoro mkubwa, ambao unaweza kusababisha maandamano ya kijamii na hata kusambaratika kwa Umoja wa Ulaya. Haya yanajiri wakati Marekani, ambayo imeiingiza Ulaya katika vita huko Ukarine ikiwa haina uwezo wa kuchukua hatua madhubuti za kuiondolea Ulaya matatizo ya nishati.

Kwa kuzingatia hali hiyo, inaonekana kwamba ikiwa hali itaendelea kama ilivyo hivi sasa; vita vya gesi vitabadilisha mkondo wa maendeleo na ustawi huko Ulaya au hata ulimwengu mzima.

Tags