Sanders aikosoa Marekani kwa kuimarisha uhusiano na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i85998-sanders_aikosoa_marekani_kwa_kuimarisha_uhusiano_na_saudia
Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani amekosoa vikali safari ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo huko Saudi Arabia na kusisitiza kuwa, Washington haipaswi kuwa na 'uhusiano mzuri' na utawala huo wa kifalme.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2022 03:07 UTC
  • Sanders aikosoa Marekani kwa kuimarisha uhusiano na Saudia

Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani amekosoa vikali safari ya Rais Joe Biden wa nchi hiyo huko Saudi Arabia na kusisitiza kuwa, Washington haipaswi kuwa na 'uhusiano mzuri' na utawala huo wa kifalme.

Bernie Sanders amesema Biden hakupaswa kuitembelea Saudia wala kukutana na mrithi wa ufalme wa utawala huo wa kiukoo, Mohammed bin Salman, anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Vyombo vya intelijensia vya Marekani vilitoa tamko rasmi la hitimisho kwamba Mohammed bin Salman ndiye "aliyeidhinisha operesheni" ya kumteka au kumuua Jamal Khashoggi, kabla ya mwandishi huyo wa habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud, kuuawa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Uturuki mwaka 2018.

Sanders katika mahojiano na kanali ya televisheni ya ABC amesema: Kiongozi wa nchi hiyo (Saudia) alihusika na mauaji ya mwanahabari wa Washington Post, sidhani kama seriakali ya namna hiyo inapaswa kupewa zawadi ya ziara ya Rais wa Marekani. 

Bernie Sanders

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa mgombea wa urais nchini Marekani amekuwa akiikosoa Saudi Arabia mara kwa mara, na hata kuwaita viongozi wa nchi hiyo kuwa ni 'wauaji na majambazi'.

Seneta huyo wa Vermont amekuwa akimesisitiza kuwa hana tatizo na raia wa Saudi Arabia, huku akimtaja mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman kuwa ni 'bilionea dikteta'.