WHO yaitangaza Monkeypox kuwa tishio la afya duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i86216-who_yaitangaza_monkeypox_kuwa_tishio_la_afya_duniani
Shirika la Afya Duniani WHO limeutangaza mripuko wa ugonjwa wa Ndui ya Nyani (Monkeypox) kuwa tishio la afya duniani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 24, 2022 07:17 UTC
  • WHO yaitangaza Monkeypox kuwa tishio la afya duniani

Shirika la Afya Duniani WHO limeutangaza mripuko wa ugonjwa wa Ndui ya Nyani (Monkeypox) kuwa tishio la afya duniani.

Hiyo ni tahadhari ya juu kabisa inayoweza kutolewa na shirika la WHO kuhusu dharura yoyote ya kiafya ulimwenguni, huku ugonjwa huo ukiwa tayari umeathiri zaidi ya watu 16,000 katika nchi 75 duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Geneva kwamba, ameamua kuitangaza Ndui ya Nyani kuwa dharura ya kiafya duniani baada ya timu ya wataalamu kushindwa kufikia makubaliano.

Amesema tathmini ya WHO inaonesha kitisho cha Homa ya Nyani duniani bado ni cha wastani isipokuwa barani Ulaya ambako visa vya maambukizi vinaongezeka. Dakta Ghebreyesus ameongeza kuwa, hadi sasa watu wasiopungua watano wamefariki dunia kutokana na maradhi hayo.

Naye Dakta Michael Ryan, Mkuu wa Idara ya Dharura ya WHO amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la afya duniani amechukua uamuzi wa kutoa tangazo hilo ili kuhakikisha kuwa jamii ya kimataifa inauchukulia kwa uzito mripuko wa sasa wa Monkeypox, ili kuzuia maambukizi zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus

Utafiti unaonesha kuwa, maambukizi ya ugonjwa huo yanaongezeka, huku asilimia 95 ya walioambukizwa wakiwa ni wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Kesi ya kwanza ya ugonjwa huu iliripotiwa kwa mara ya kwanza huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika muongo wa 70 na kuenea kutoka mnyama hadi kwa mwanadamu baada ya kukaribiana. Kwa mujibu wa WHO, chanjo zilizotumika wakati wa kutokomeza ndui, zilitoa pia kinga dhidi ya Monkeypox. Hata hivyo chanjo mpya zimebuniwa na moja imethibitishwa kukinga Monkeypox.